RAIS SAMIA AWEKEZA MIRADI MINGI YA MAJI NA AFYA KUWASAIDIA WANAWAKE NCHINI : RC MAKALLA
*Asema nchi imetulia, Rais Samia ni wa kuigwa kwa Demokrasia*
*Atoa wito kwa NGO's kuendelea kupinga ukatili wa kijinsia*
*Wanawake wakandarasi wapewe haki sawa kwenye kuteleza miradi*
*Madawati ya kupinga ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yote yawepo*
*Maambukizi ya VVU yafikia 7.2 waathirika zaidi ni wanawake na wasichana*
*Mikopo ya Wanawake itarejea, Serikali inaandaa utaratibu*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amesema kuwa upatikanaji wa maji mkoani Mwanza utafikia asilimia 86 kutoka 70 ya sasa vijijini ifikapo mwaka 2025 kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwenye miradi ikiwa ni katika kuhakikisha wanawake wanaondolewa adha hiyo.
CPA Makalla amebainisha hayo leo, Machi 08, 2024 alipokua akihutubia wanawake wa Mkoa wa Mwanza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa kwenye viwanja vya Amani wilayani Misungwi.
Makalla amesema Rais Samia amekua akitoa fedha nyingi kwenye miradi mathalani zaidi ya Bilioni 30 kwenye mradi wa kata ya Kolomije wilayani Kwimba ambapo anakusudia kuwatua wanawake ndoo kichwani na akabainisha kuwa mikopo kwa Wanawake itarejea na sasa Serikali inaandaa utaratibu mzuri wa kutoa.
Aidha, ametoa wito kwa wakuu wa wilaya pamoja na asasi zisizo za kiserikali kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwa wananchi ili iwe na ufahamu na kuweza kujilinda na kuwa na ujasiri wa kuripoti waonapo madhila ya aina hiyo kwenye jamii.
Akizungumzia maambukizi ya virusi vya ukimwi yaliyofikia asilimia 7.2 amebainisha kuwa Mkoa huo unaendelea na mikakati ya kuondokana na madhila yanayopelekea maambukizi kuwa juu na akawataka wazazi kuzingatia malezi bora ya watoto kwenye kaya zao.
"Mkoa wetu una viongozi wanawake kwa ngazi mbalimbali mathalani Wakuu wa Wilaya watatu tena wanachapa kazi vizuri pia tunaye MNEC, mkurugenzi wa mamlaka ya maji ya mkoa tena amekua kinara katika kuendeleza mkakati wa kumtua mama ndoo kichwani." Makalla.
Akitoa salamu za wanawake mkoa wa Mwanza Mwenyekiti wa jamati ya maadhimisho hayo Zeyana Seif amesema ameiomba Serikali kuongeza shule za bweni kwenye shule za sekondari ili kundi hilo lipate mazingira mazuri ya kupata elimu na kupumzika badala ya kutembea umbali mrefu na kukutana na vishawishi.
"Ongezeko la watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, matumuzi ya dawa za kulevya, mimba za utotoni, ukatili pqmoja na watoto wa mtaani ni miongoni mwa matokeo ya wanawake kujikita kwenye utafutaji na kujihusisha na shughuli za uchumi hivyo tunaiomba Serikali irejeshe nfuko wa uwezeshaji kwa wanawake." Bi. Zeyana.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Mkoa wa Mwanza Mhe. Adela Mayengela ametoa wito kwa wanawake kuisherehekea siku hiyo kwa dhati huku wakijiamini lakini akawakumbusha wajibu wa kuhakikisha wanachapa kazi ili kuliletea Taifa maendeleo na kumuunga mkono Rais Samia.
Jackline Aluta kutoka Shirika la Aman Girls Foundation amesema Shirika hilo kupitia mradi wa Afya, Elimu na uhifadhi wa jamii wanahakikisha wanawalinda mabinti kuanzia rika la umri balehe ili waweze kufikia ndoto zao kwa kupata elimu na sio kuingia kwenye masuala ya ngono.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.