RAS BALANDYA AAHIDI KUWAPA FURSA ZAIDI WATUMISHI ILI KUONGEZA UFANISI WA KAZI
Katibu Tawala wa mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana ameahidi kutoa fursa zaidi kwa watumishi wa Ofisi ya mkuu wa mkoa kadiri ya uwezo wa fedha itaporuhusu ili kuongeza ufanisi wa kazi.
Ametoa kauli hiyo leo Alasiri Machi 3, 2025 Ofisini kwake wakati wa hafla fupi ya kupokea zawadi kutoka kwa watumishi waliokwenda ziara ya kutembelea Bwawa la umeme la Mwl. Nyerere na Treni ya kisasa ya SGR.
Amesema, mpango huo kwa watumishi una gharama lakini ofisi itaendelea kujibana ili kufanikisha hilo akiamini mazingira mazuri kwa watumishi kama hayo ndiyo kichocheo cha kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Serikali ya awamu ya sita imefanya mengi hasa miradi mikubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo, naamini ziara yenu imewafanya kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi na hata kwa familia zenu kurudi kuwatembeza", amesisitiza Balandya.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi hao kabla ya kumkabidhi ndugu Balandya zawadi ya suti na picha ya pamoja ya watumishi wakiwa eneo la mradi wa umeme, Afisa Utumishi na Rasilimali watu Paul Cheyo amemshukuru mtendaji huyo wa Mkoa kwa kutoa nafasi hiyo kwa watumishi ambayo imewaongezea mambo mbalimbali hasa mshikamano ya kufanya kazi kwa ari.
"Ndugu Katibu Tawala uamuzi wako ni wa busara na umeona mbali sana,sisi watumishi tunatumia muda mwingi sana kuwahudumia wananchi, wakati mwingine tunakosa hata mapumziko tunakuahidi kuleta matokeo chanya baada ya ziara hizi kwa kuchapa kazi kwa bidii," Cheyo.
Watumishi kutoka Ofisi ya Mkoa wa Mwanza kwa nyakati tofauti wamepata fursa ya kutembelea kwa awamu mbuza za wanyama Serengeti na Ngorongoro na wengine kutembelea Bwawa la umeme la Mwl Nyerere na Treni ya kisasa ya SGR.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.