RAS BALANDYA AFANYA ZIARA YA GHAFLA KITUO CHA AFYA IGOMA, AWAPONGEZA WATUMISHI
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana usiku wa Jumapili Septemba 8,2024 amefanya ziara ya ghafla kwenye kituo cha afya Igoma na kuridhishwa na utendaji kazi wa watumishi waliokuwa zamu muda huo na kuwataka kuongeza bidii ya kuwatumikia wateja wao.
Akiambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Jesca Lebba,Balandya alianzia sehemu ya mapokezi ya wagonjwa kutoka nje OPD na kufanya mazungumzo nao namna walivyopokelewa na utaratibu mzima waliopatiwa kituoni hapo huku kila mteja akipongeza huduma sahihi walizopata.
Mtendaji huyo wa Mkoa alipita sehemu za wodini na wodi ya wazazi na huko pia alizungumza nao kabla ya kukagua sehemu ya kutolea dawa na kila eneo alishuhudia madaktari wa zamu na wasaidizi wao wakiendelea na kazi.
"Nawaombeni msiingie shaka kwa ujio huu na hasa kwa muda kama huu wa usiku, hii ni sehemu ya wajibu wetu kama viongozi na niwapongeze kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wateja wenu,"amesema Balandya wakati akizungumza na watumishi wa kituo hicho na baadhi kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu.
Balandya amebainisha mara ya mwisho alipofanya ziara kwenye kituo hicho alipewa taarifa za changamoto mbalimbali za kiutendaji ukiwemo upungufu wa watumishi na uboreshaji wa mazingira ya kazi ambayvyo vyote vimefanyiwa kazi na mengineyo yapo mbioni kuboreshwa kulingana na bajeti ya Serikali.
Daktari wa zamu wodi ya wazazi,Mwita Chacha amesema wateja wake aliowapokea amawafanyia uchunguzi na wapo katika hali nzuri, na baadhi amewapa maelekezo ya kufanya mazoezi ili kurahisisha mzunguko wakati wa kujifungua
"Nampongeza Mganga Mkuu wa mkoa kwa kazi nzuri tangu umefika kituo chako kipya cha kazi hapa Mwanza sasa ni miezi miwili lakini umezunguka Halmashauri zote ili kujionea utendaji kazi na kutoa maelekezo," Balandya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Jesca Lebba amesema yeye na timu ya wataalamu kutoka Ofisini kwake wameweka utaratibu wa kufanya ukaguzi na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa watumishi wa vituo na hospitali zote za Serikali ili kuhakikisha kunakuwa na muendelezo wa utolewaje mzuri wa huduma bora kwa wateja wao.
"Ndugu Katibu Tawala, Mkoa wetu umekuwa hauna rekodi nzuri katika uzazi wa mama mjamzito,tumejipanga vizuri kuhakikisha vifo vinatoweka kwa kiwango kikubwa kama ulivyojionea madaktari wa zamu wapo muda wote wodi ya wazazi na wote wamefanyiwa uchunguzi na wenye changamoto zimefanyiwa kazi ili wajifungue salama,"Dkt.Lebba
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.