Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana amewataka Wadau wa Dawati la ulinzi na Usalama kwa Mtoto kuhakikisha Elimu hiyo inaleta Matokeo chanya ndani ya Jamii kwa kuifanyia kazi kwa vitendo ili kutokomeza ukatili.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu Ndugu Daniel Machunda kwa niaba ya Katibu Tawala wakati akifungua mafunzo ambapo amesema wadau wa Maendeleo Plan International wamefanya uamuzi mwafaka wa kuwezesha mafunzo hayo kutokana na changamoto hiyo inayoikabili Jamii.
"Nawapongeza sana Plan International mmekuwa bega kwa bega na Serikali katika kumletea maendeleo mwananchi, sisi kama Serikali tunawaahidi kuendelea kushirikiana nanyi kwenye kila Sekta" amesema Machunda
Aidha, Kaimu Katibu Tawala huyo amesema Mkoa umekuwa ukitekeleza mpango kazi wa Taifa wa Mkakati wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto MTAKUWWA kwa kuelimisha Jamii kufahamu umuhimu wa kushiriki kwenye shughuli za Maendeleo yakiwemo ya Jinsia, Wanawake na Watoto.
Mratibu wa mafunzo hayo Bi. Bernadetha Mazura amebainisha mafunzo hayo yanatolewa hasa baada ya kubaini rekodi isiyoridhisha ya vitendo vya ukatili kwa watoto inayochangiwa na Jamii kukosa elimu ya kutosha.
"Ndugu mgeni rasmi, tunashuhudia vitendo vingi vya ukatili kwa watoto yakiwemo mauaji na ubakaji hivyo tukiwekeza vya kutosha kwenye kutoa elimu kwa Jamii kutaleta mabadiliko," amesisitiza Bi. Bernadetha.
Mafunzo hayo kuanzia ngazi ya Kata, Wilaya na Mkoa yamewashirikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, Waratibu elimu pamoja na Dawati la Jinsia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.