RAS Balandya ashauri Asasi za kiraia kushikamana kuelimisha jamii kutokomeza ukatili wa kijinsia
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana amezishauri Asasi za kiraia kushirikiana kwa pamoja katika kuongeza kasi ya uelimishaji kwa jamii kuhusiana na ukatili wa kijinsia huku wahanga wakubwa wakiwa ni watoto, wasichana na wanawake.
Akizungumza leo katika Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwenye ukumbi wa mikutano wa M 14 uliopo chuo kikuu cha Mt. Agustino, Mtendaji huyo wa Mkoa amebainisha licha ya sheria za kupambana na hali hiyo kuwepo ikiwemo Ile ya Maudhui mtandaoni 2020 bado vitendo vya ukatili wa kijinsia vimekuwa vikifanyika.
"Wahanga wengi wamekuwa wakinyamazia vitendo hivyo kwa hofu na kuamini kuwa watadhalilika zaidi endapo suala lake litafikishwa kwenye vyombo vya sheria", amefafanua Balandya wakati akizungumza na washiriki wa Maadhimisho hayo wengi wakiwa ni mawakili na wanachuo wanaosomea sheria.
Balandya amezipongeza Asasi hizo za kiraia kwa kushirikiana na Serikali kwa kupunguza vitendo hivyo kwani takwimu zimeonesha mwaka 2016 ilikuwa asilimia 60 na mwaka 2022 asilimia 47.
"Ndugu mgeni rasmi kwa kutambua umuhimu wa jamii kuelimika hasa uhuru uliopo sasa mitandaoni,mahakama itaendelea kutoa elimu na kuepuka aina yoyote ya hofu kwa wahanga",Mhe. Stanley Kamanya,Jaji Mfawidhi Kanda ya Mwanza.
"Kuongezeka kwa matumizi ya Teknolojia ni dhahiri wahanga wakubwa wamekuwa ni wasichana na wanawake na madhara yake ni kushindwa kushiriki kikamilifu katika masuala ya kiuchumi na kugubikwa na msongo wa mawazo na mwishowe baadhi yao kuchukua maamuzi mabaya ya kujiua,"Mhe.Lilian Temba,Jaji wa Mahakama kuu Kanda ya Mwanza.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Saut,Dkt.Neema Mwita aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa chuo amebainisha Saut imekuwa na mchango mkubwa kwa kuwatoa wataalamu wa sheria ambao wamekuwa chachu ya kutoa msaada wa kisheria kwa jamii.
Katika Maadhimisho hayo washiriki wamepata wasaa wa kuona mfano wa Mahakama zinavyo fanya kazi katika kuendesha kesi za ukatili wa kijinsia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.