RAS Balandya atembelea maeneo hatarishi na Kipindupindu na kutoa maagizo
*Awaagiza Wavuvi wa Mwalo wa Mihama kuimarisha miundombinu ya Maji taka*
*Awataka Maafisa afya kuwachukulia hatua kali wasiokuwa na vyoo bora*
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana leo Februari 14, 2024 amefanya ziara fupi ya kutembelea maeneo yaliyokumbwa na ugonjwa wa Kipindupindu Mihama kata ya Kitangiri na Kabuhoro-Kirumba na kuwataka maafisa afya kuwachukulia hatua za kinidhamu wale watakaobainika kutozingatia kanuni za usafi kwenye maeneo yao.
Mtendaji huyo wa Mkoa aliyeambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa Thomas Rutachunzibwa pamoja na Maafisa wa afya kutoka Halmashauri ya Ilemela amebaini kasoro kadhaa ikiwemo ukosefu wa choo bora na kutokuwepo kwa vifaa vya kunawa mikono licha ya eneo hilo kuwa na muingiliano wa watu wengi.
"Ndugu zangu nimefika hapa na kujionea hali isiyoridhisha, nawaagiza viongozi wote kwenye eneo hili rekebisheni haraka kasoro zote mkianzia miundombinu ya maji taka na vifaa vya kunawa mikono," amesisitiza Balandya wakati akizungumza na wakazi wa eneo hilo wengi wao wakiwa ni wavuvi.
Amewataka Maafisa afya kuwa wakali na kuchukua hatua bila kusita kwa wanaokwenda kinyume na miongozo iliyotolewa na kuzidi kutoa elimu kwa wananchi.
"Nimetembelea kaya kadhaa maeneo haya ya Mihama nimeona wasivyo zingatia usafi na nyumba nyingi hazina vyoo bora na nyingine hazina kabisa hii ni hatari na kukwamisha zoezi la kutokomeza ugongwa wa Kipindupindu," Katibu Tawala mkoa
Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Thomas Rutachunzibwa amesema Ofisi yake imejipanga kuudhibiti ugonjwa huo na kuwataka watumishi wengine kuongeza bidii katika maeneo yao ili kudhibiti maambukizi.
"Ndugu Katibu Tawala hii ni vita na jiografia ya Jiji letu wakazi wengi wapo maeneo karibu na mialo na milimani hivyo siyo sawa kuiwachia Idara ya afya pekee kupambana na hili, Maafisa uvuvi, MWAUWASA,TARURA na wengineo ni lazima kila mmoja awajibike ipasavyo katika eneo lake naamini tutafanikiwa," Dkt. Rutachunzibwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.