Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amewataka mafundi sanifu kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa lakini pia wawe waadilifu ili waweze kutekeleza miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali kwa kiwango kilichokusudiwa.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa tano wa mwaka wa mafundi sanifu uliowakutanisha washiriki zaidi ya 500 kutoka mikoa mbalimbali nchini unaofanyika jijini hapa kuanzia leo Mei 4 hadi 5,2023, Elikana amesema miradi yote inayotekelezwa na serikali kuna mchango mkubwa wa mafundi sanifu ambao wanaiwezesha kuendelea hivyo ni vyema wakawa waadilifu katika kutimiza majukumu yao.
“Naipongeza sana serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwaletea wananchi maendeleo, katika mkoa wetu wa Mwanza tumekuwa tukipokea mabilioni ya shilingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ya maendeleo.
“Tuna miradi ya kimkakati ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa daraja la JPM Kigongo- Busisi, reli ya kisasa, ujenzi wa meli mpya kubwa ya aina yake katika ukanda wa maziwa makuu MV MWANZA HAPA KAZI TU stendi ya mabasi ya abiria Nyegezi na mingine mingi inayotekelezwa na Tanroads na Tarura na hivi juzi tumesaini mkataba kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kilomita 54 kutoka Sengerema hadi Buchosa yote hii tunawategemea nyie mafundi sanifu,” amesema Elikana na kuongeza
“Ni matumaini yetu miradi hiyo itakapokamilika itachochea sana ukuaji wa uchumi wa mkoa wetu, kanda ya ziwa na nchi kwa ujumla, tunaishukuru sana serikali lakini pia tunawategemea nyie mafundi sanifu mfanye kazi kwa bidii na muwe waadilifu ili tuweze kuitekeleza miradi hiyo na ionyeshe thamani halisi ya fedha,”ameeleza Elikana.
Katika hatua nyingine Katibu Tawala huyo wa Mkoa wa Mwanza aliwasihi washiriki wote wa mkutano huo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo mkoani humo kabla hawajaondoka.
“Mkoa wetu wa Mwanza umejaliwa kuwa na vivutio vya aina mbalimbali na vya kipekee vya utalii ikiwa ni pamoja na fukwe nzuri zilizopo katika ziwa Viktoria, utalii wa majini, hifadhi ya taifa ya kisiwa cha saa nane na vivutio vya utalii vya utamaduni vilivyopo katika makumbusho ya utamaduni ya wasukuma buchosa,”amefafanua na kuongeza
“Pia Mkoa wetu wa Mwanza umezungukwa na visiwa, Wilaya ya Ukerewe tu inavisiwa takribani 38 visiwa vya ukerewe vina mambo mengi mazuri, kuna kisiwa cha ukara ambacho kina jiwe linalocheza,”amebainisha Katibu Tawala Elikana.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi kwenye mkutano huo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi sekta ya Miundombinu, Balozi Mhandisi Aisha Salim Amour ameielekeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi nchini(ERB)kupeleka serikalini mpango mkakati utakaotatua changamoto za uhaba wa mafundi sanifu ikiwa ni pamoja na kuboresha mfumo wa elimu na ajira.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.