Katibu Tawala Msaidizi, Seksheni ya Miundombinu Mkoa wa Mwanza, Msanifu wa Majengo Chagu Ng'homa ameonya kuwa wakandarasi ambao hawatakidhi Sifa zinazohitajika hawatapata kazi za Ujenzi wa Miradi ya Maendeleo Mkoani humo huku akiwataka watakaopata kutekeleza kwa mujibu wa mikataba yao.
Amesema hayo leo katika Kikao Kazi cha Wahandisi kutoka Sekta ya Barabara (TARURA) na Majengo kutoka kwenye Halmashauri za Mkoa huo kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa Balandya Elikana walichoketi kufanya tathmini ya miradi iliyotekelezwa mwaka wa fedha uliopita na itakayotekelezwa 2022/23.
"Hali ya utekelezaji wa miradi mkoani Mwanza tunajivunia maana miradi mingi imeenda vizuri na leo tumekuja kuwekeana mikakati ya kuendelea kuboresha zaidi miradi yetu kwa mwaka huu na ili tufanikishe haya ni lazima tuwe na weledi kwenye Utekelezaji wa miradi hivyo tunazingatia" Amesema Ng'homa.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Goodluck Mbanga amesema kuwa bajeti ya kutekeleza miradi ya barabara Mkoani humo imekua ikiongezeka kila mwaka huku akibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/23 imetengwa zaidi ya Shilingi Bilioni 25 na kuna mikataba zaidi ya 90 itatekelezwa tofauti na 2021/22 ilipotekelezwa mikataba 43.
Bi. Maua Ally, Afisa Mahusiano na Elimu kwa Umma kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wakati akitoa Mada ya Maadili na Changamoto za Rushwa kwenye utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa niaba ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza amesema thamani ya fedha kwenye miradi ya ujenzi ni lazima ionekane ili wananchi wapate miradi bora itakayodumu kwa muda mrefu.
Ameongeza kwa kuwasihi wahandisi kufanya kazi kizalendo na kutojihusisha na vitendo vya Rushwa kwa namna yoyote kwani haina manufaa bali ni dhuluma na dhambi kwa mwenyezi Mungu na kwamba mtu akijihusisha nayo ataharibu kizazi chake kwani tabia hiyo inarithi kwenye vizazi hadi vizazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.