Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amewasihi wataalamu wa Maabara nchini kuhakikisha wanazingatia msingi na kuwa na weledi wa kitaalamu wanapofanya uchunguzi na vipimo ili kupata matokeo sahihi na kupelekea matibabu halisi kwa wagonjwa.
Ametoa wito huo leo tarehe 25 Septemba, 2025 wakati akifungua Mkutano wa 38 wa Jumuiya ya Wataalamu wa Sayansi Maabara (MeLSAT) kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya nchini uliowakutanisha wataalamu zaidi ya 600 kutoka ndani na nje ya nchi katika Ukumbi wa Kwa Tunza Beach uliopo Ilemela mkoani Mwanza.
Amesema, ni lazima wanataaluma wa Sayansi ya Maabara kuhakikisha wanazingatia sheria za taaluma zao na kukiepusha na matendo ya rushwa na ubatili mwingine wowote ili kuhakikisha majibu ya uchunguzi yanakua halisi na kuweza kutoa matibabu yanayostahili kwa wagonjwa.
“Maabara ndio uti wa mgongo wa matibabu kwasababu kabla ya mgonjwa kupata tiba ni lazima afanyiwe uchunguzi na vipimo ndipo abainike anaumwa nini na kupatiwa tiba hivyo nawasihi mhakikishe mnakua kiungo bora cha matibabu nchini ili tupate taifa lenye watu wenye afya nzuri.” Amesisitiza Katibu Tawala.
Aidha, ametoa wito kwa wataaluma wa maabara kujiunga na kuzingatia katiba yao katika kulipa ada na kuwa wanachama hai ili ikiwezekana wanachama wote elfu 16 wawe katika mwamvuli mmoja tofauti na ilivyo sasa ambapo ni elfu 6 pekee wamejiunga na akatoa rai kwao kushiriki kwenye makongamano.
“Wana taaluma wote wa maabara naomba niwasihi, kama mnataka kufika mbali kwa pamoja ni lazima muwe wengi na wamoja hivyo nawaombe mjiunge kwenye chama chenu (MeLSAT) na waajiri nchini muwawezeshe kushiriki katika vikao vya kitaaluma kuanzia kwenye uandaaji wa bajeti.” Amesema, Balandya.
Raisi wa Chama hicho cha MeLSAT Bw. Yahya Mnung’a amesema wanachama katika kongamano hilo pamoja na mambo mengine watajadili changamoto na mafanikio ya taaluma yao na matumizi ya akili unde na athari zinazoweza kuathiri taaluma hiyo na kuweka mikakati ya kukabiliana na matokeo hasi ya teknolojia hiyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.