RAS Balandya awatangazia wastaafu watarajiwa wa mfuko wa PSSSF fursa zilizopo Mwanza
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana amewashauri wastaafu watarajiwa wa mfuko wa PSSSF kuchangamkia fursa zilizopo Mwanza ukiwemo mgodi wa Nyanzaga uliopo Wilayani Sengerema.
Mtendaji huyo wa Mkoa ametoa kauli hiyo leo Jijini Mwanza kwenye ukumbi wa Rock City Mall wakati wa ufunguzi wa semina ya siku mbili ya wastaafu watarajiwa ambapo amesema mgodi huo unaotarajia kuanza kazi hivi karibuni utahitaji huduma mbalimbali hivyo ni eneo mwafaka la kujipatia kipato.
"Ndugu zangu wastaafu watarajiwa tumieni semina hii mpate kuelimika vizuri ili iwe na tija kwenu siku za baadaye,mgodi wa Nyanzaga ambao ni pili kwa ukubwa baada ya Geita utahitaji huduma nyingi kama vyakula hivyo ukijikita kwenye ufugaji bora utaweza kusambaza mayai au nyama,"Balandya
Ameongeza kuwa rasilimali ya maji ya ziwa Victoria pia ni eneo lingine la uwekezaji kama ufugaji wa kisasa wa samaki kwa njia ya vizimba au uvuvi kwa kutumia boti za kisasa zilizotolewa na Serikali.
Ameupongeza pia mfuko wa PSSSF kwa utaratibu wa kutoa semina hiyo kwenye mikoa mbalimbali ambayo inawasaidia wastaafu hao watarajiwa kujengewa uwezo kwani baadhi yao huishia kutapeliwa au kujikuta wakifanya maamuzi yasiyo sahihi ya matumizi ya fedha zao.
"Baadhi ya wastaafu wamejikuta wakipatwa na maradhi au kuchanganyikiwa na wengine kupoteza maisha kutokana na walichotarajia kiwasaidie kimetumika ovyo na kujiweka katika hali ya umasikini,hivyo naamini kupitia jukwaa hili mtaelimika vyema na fedha zenu kuwa salama kwa muda wote wakati wa kustaafu",amesisitiza Mtendaji huyo wa Mkoa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa PSSSF Bi.Vupe Ligate amebainisha lengo la semena hiyo ni kuhakikisha wateja wao wanakuwa na maamuzi sahihi ya matumizi ya fedha zao pale wanapoamua kujishughulisha na miradi mbalimbali ya kujiongezea kipato kwa familia,ndiyo maana kwenye semina hiyo wapo wataalamu wa fani mbalimbali watakao toa elimu pamoja na Taasisi za kifedha zenye wajibu wa kutoa mikopo na kutunza fedha hizo.
"Ndugu mgeni rasmi hapa tunao wataalamu wa ufugaji nyuki,wachumi na wengineo ambao kwa siku mbili watatoa elimu kwa wateja wetu ambayo itakuwa ni dira mwafaka kwao utakapo fika muda wa kuamua kipi cha kufanya,"Bi.Ligate.
Kauli mbiu ya semina hiyo inasema "Wekeza Mafao yako sehemu salama kwa uhakika wa Ukwasi".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.