RAS MWANZA AAHIDI USHIRIKIANO ZAIDI NA TASAF
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amesema Mkoa huo utaendelea kushirikiana na mpango wa Taifa wa kunusuru kaya masikini nchini (TASAF) ili kuendelea kuwainua wananchi kiuchumi na kuwatoa katika umasikini.
Amesema hayo mapema leo Januari 27, 2025 ofisini kwake wakati akiongea na ugeni kutoka TASAF makao makuu ulioambatana na washirika wa maendeleo kutoka Benki ya Dunia pamoja na Ubalozi wa Sweden.
Balandya amesema, Mwanza inajivunia miradi inayotekelezwa kama kutoa fursa kwa jamii za kujiongezea kipato na kuboresha huduma za kiuchumi kwa kaya za walengwa na kulinda maslahi ya watoto hivyo wataendelea kushirikiana na TASAF kila uchwao kuhakikisha malengo yanafikiwa.
Aidha, amewashukuru TASAF kwa uhawilishaji fedha ambapo amebainisha kuwa umesaidia kuongeza kipato cha kaya na kuwekeza katika afya na elimu ya watoto pamoja na kuinua uchumi wa kaya kwa kujenga uwezo kwa kaya katika utunzaji rasilimali na kutengeneza njia mbadala na endelevu za ajira.
Vilevile, ametoa wito kwa mfuko huo kuendelea kusadia juhudi mbalimbali za Serikali kama kuondoa magugu kwenye ziwa victoria ambayo yamekua yakisababisha kuharibu vivuko na kusababisha adha ya usafiri kwenye visiwa na vivuko kati ya pande mbili zinazosafiri.
Japhet Boaz, akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ametumia wasaa huo
kupongeza na kuwashukuru viongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na watendaji wao katika kutekeleza miradi kwa ufanisi.
Ugeni huo upo Mkoani Mwanza kwa siku tatu kwa ajili ya kutembelea miradi ili kuangalia utekelezaji wa mpango huo na mafanikio hususani katika Manisapaa ya Ilemela.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.