RAS Mwanza ahimiza juhudi zifanyike kutokomeza Uvuvi Haramu Ziwa Victoria
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amezitaka Asasi zisizo za Kiserikali kuendelea kushirikiana na Serikali kutokomeza uvuvi haramu Ziwa Victoria ili sekta hiyo iendelee kuchangia uchumi wa mtu mmoja mmoja na pato la Taifa.
Akifungua leo kikao cha utambulisho wa mradi wa kuzuia kuzama maji Ziwa Victoria unaosimamiwa na Shirika linalojihusisha na mazingira na uvuvi la EMEDO kwenye ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Balandya amebainisha bado kumekuwepo na kesi nyingi za wavuvi zinazotokana na Uvuvi haramu ikiwemo utumiaji wa nyavu zisizo stahili na njia mbaya za ulipuaji kuwapata samaki.
"Nawapongeza Shirika lisilo la Kiserikali la EMEDO mnao jihusisha na mazingira na Uvuvi kwa kujikita kwenu mradi huu kwenye Wilaya mbili za mkoa huu za Ukerewe na Nyamagana,nina imani malengo yenu ya kuzuia majanga ya kuzama maji yatapungua au kumalizika kabisa",amesisitiza Mtendaji huyo wa Mkoa wakati akizungumza na washiriki wa kikao hicho wakiwemo maafisa uvuvi,Tasac,TMA, na Maabara ya Taifa ya samaki.
Balandya amesema sekta ya uvuvi kwa Mkoa wa Mwanza inachangia asilimia 7 ya pato la Mkoa,lakini majanga ya wavuvi kuzama na kupoteza maisha yamekuwa yakitokea mara kwa mara,hivyo mkazo wa elimu hauna budi kutolewa ili wafanye shughuli zao kwa usalama.
Meneja mradi kutoka EMEDO Arthur Mgema amesema mwaka 2021 walianza kufanya utafiti wa sababu za majanga ya kuzama maji kwa Wilaya nne za Ukerewe,Nyamagana,Muleba na Musoma vijijini na kubaini changamoto mbalimbali.
"Miongoni mwa sababu za majanga ya kuzama ni elimu ndogo za wavuvi,uelewa hafifu wa hali ya hewa pamoja na ulevi, na utafiti huu umewalenga makundi manne ambayo ni wavuvi,watoto,wachakataji na bodaboda wanaobeba samaki kutoka kwenye mialo",Mgema.
Mradi huo ulioanza mwaka 2022 utamalizika mwaka 2025 ukijikita kwenye mikoa ya Mwanza,Kagera na Mara yenye shughuli kubwa ya uvuvi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.