Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amewataka watendaji wa Afya kuhakikisha wanalinda afya ya mama na mtoto kwa kusimamia vifaa vya kujifungulia na kuhakikisha vinakuwepo vituoni muda wote, ikiwa ni pamoja na uimarishaji wa mfumo wa kumfuatilia mama mjamzito sambamba na maandalizi ya kujifungua.
Bwana Elikana ameyasema hayo wakati akizungumza katika kikao cha Robo Mwaka cha watendaji wa Sekta ya Afya kwa ajili ya kujadili Vifo vya mama vinavyotokana na uzazi pamoja na vifo vya watoto wachanga kilichofanyika katika Wilaya ya Misungwi.
"Simamieni vifaa vya kujifungulia viwepo vituoni muda wote, Serikali imeendelea kutoa fedha za dawa na vifaa tiba kupitia MSD," amesena Elikana.
Aidha, amesisitiza kuwa asingependa kusikia mama au mtoto amekosa huduma kwa kisingizio cha kukosa dawa, na kutoa angalizo kuwa, mojawapo ya vipaumbele vya Serikali kupitia Sekta ya Afya kwa mwaka 2023 ni ubora wa huduma.
Pamoja na msisitizo wa huduma bora za afya Bw.Elikana amewataka watendaji kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Bima ya Afya kwa wote na kusimamia utekelezaji ili elimu ya Bima ya Afya itolewe kwa wananchi kupitia vituo vya kutolea huduma za afya na katika mikusanyiko kadri inavyowezekana.
"Hili ni eneo la kipaumbele kwa Serikali linalolenga kuondoa kizingiti cha kutokuwa na fedha kwa wananchi katika kupata huduma ya Afya,"amesisitiza Elikana.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa amebainisha wamepokea maelekezo ya Katibu Tawala na kuanza kuyafanyia kazi na wamejipanga imara kuhakikisha Sekta ya Afya inazidi kuwa na matokeo chanya kwa kuzingatia uwepo wa vifaa tiba na huduma bora.
Hata hivyo Bw. Elikana amewakumbusha kuwa Majengo yaliyoelekezwa kujengwa yakamilishwe na yaanze kutumika mara moja, RMO na DMO wahakikishe wanasimamia ili vituo vikamilike kwa wakati,visajiliwe na vianze kutoka huduma kwa wananchi kwani Serikali imewekeza fedha nyingi katika huduma za afya.
Katibu Tawala amewapongeza Sekta ya Afya kwa utaratibu wa kufanya vikao kama hivyo vya kujadili changamoto za Kiafya zinazozikabili jamii.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.