Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ngusa Samike ametoa rai kwa viongozi na watendaji mkoani humo kutoa elimu ya matumizi sahihi na usambazaji wa Makasha ya Kondomu kwa jamii ili kujikinga na maambukizi ya Ukimwi.
Akizungumza kwa niaba yake,Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji Mkoani Mwanza Emil Kasagara amesema hayo leo wakati akifungua kikao kazi cha Usambazaji wa Mkakati na Mwongozo wa Taifa wa Kondomu kilichofanyika katika Ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa watendaji wa mitaa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza.
"Niwaombe tukafikishe elimu hii kwa jamii, hakikisheni tunatoka na majibu ya namna gani kondomu zitawafikia wananchi wote maana sifa yetu Mwanza ni kufanya vizuri kwa hiyo twende tukashirikiane kuhakikisha kondomu zinawafikia maeneo ya vijijini. "
"Lengo la kuwa hapa nanyi ni kuwajengea uwezo ili kuhakikisha kondomu zinafika kwenye jamii na tunatoa elimu ya matumizi sahihi, hivyo Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya waziri Mkuu tunahakikisha malengo hayo yanatimia." amesema Dktr. Emmanuel Mihayo, Mratibu wa kondomu Wizara ya Afya (NACP)
Mratibu wa Kondomu kutoka TACAIDS Dktr Hafidh Ameir amesema mpango huu ni kwa Mikoa 8 ambayo imeonesha inahitaji mkazo wa elimu hiyo na mpango wa kuzungukia nchi nzima utafanyika.
"Wengine wanapuuzia wakidhani UKIMWI haupo lakini ni vizuri wana semina tukasikiliza kwa makini ili tukatoe elimu kwa wananchi dhidi ya janga hili ambalo kwa muda mrefu halina tiba." Amesema, Naibu Meya wa Jiji la Mwanza Mhe. Rodrick Ngoye.
Kikao kazi hicho kinafanyika kwa siku mbili lengo likiwa ni kuwajengea uwezo Wataalam wa Sekta ya Afya, Watendaji wa Serikali za Mitaa pamoja na Madiwani kutoka Wilaya za Nyamagana na Ilemela kupambana na ugonjwa wa Ukimwi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.