RAS MWANZA ATOA WITO KWA WADAU WA AFYA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUSAIDIA SEKTA HIYO
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza ndugu Balandya Elikana ameipongeza Idara ya Afya Mkoani humo kwa ufanisi kwenye kazi kwa kushirikiana na wadau jambo linalofanya Mwanza iendelee kuwa salama wakati wote pamoja na uwepo wa hatari ya magonjwa ya mlipuko.
Ametoa pongezi hizo leo tarehe 07 februari, 2025 wakati akifungua kikao cha Wadau wa Afya kilichoketi kwenye Ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa madhumuni ya kukumbushana wajibu katika kuhudumia jamii ili iendelee kuwa salama.
Aidha, amebainisha kuwa Mkoa wa Mwanza umejipanga kukabiliana na magonjwa ya Mlipuko kama Marburg pamoja na kuendelea kutoa huduma bora za afya kwa kushirikiana na wahisani wa ndani kutokana na kujitoa kwa baadhi ya mataifa tajiri.
Amesema, Mwanza imeshaandaa kikosi kazi cha watumishi wa afya zaidi ya 264 ambao wamepewa mafunzo maalumu ya mapambano ya ugonjwa huo na jinsi ya kumhudumia mgonjwa atakayeambukizwa na akatoa wito kwa wadau kuunga mkono juhudi hizo kwa rasilimali zozote zitakapohitajika.
Halikadhalika, ametoa wito kwa wadau kushirikiana na serikali katika kuhudumia watumishi zaidi ya 600 waliokua kwenye ufadhili wa mashirika wahisani kutoka nje ili huduma za msingi zisikwame kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Naye, Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amebainisha kuwa idara ya Afya mkoani humo wameamua kukutana na Wadau pamoja na mambo mengine ili kupitia maandalizi ya bajeti 2025/2026 na kuandaa mpango kazi wa mwendelezo wa kazi za afya baada ya baadhi ya wahisani wa nje kujitoa kwenye ufadhili.
Kaimu mratibu wa magonjwa ya milipuko Dkt. Gabriel Mashauri amesema Marburg ni ugonjwa wa mlipuko unaosababishwa na virusi vya Marburg na unaambukizwa kwa haraka kupitia njia ya damu, mate, mkojo, jasho, choo kikubwa, matapishi, maji ya uzazi na hata kugusana na dalili zake ni kutokwa damu mwilini.
Amefafanua kuwa wafanyakazi wa Afya wapo kwenye hatari zaidi ya kuambukizwa na uwezekano wa kifo hutofautiana kati ya 24% hadi 88% hivyo ni ugonjwa hatari unaosababisha vifo kwa haraka hivyo basi watu wanapaswa kuelimishwa kutochangia nguo au vitu vyenye ncha kali.
Aidha, Dkt. Mashauri amezitaja dalili za mtu aliyepata na maambukizi hayo kuwa ni pamoja na kuumwa kichwa, homa, maumivu ya misuli, mwili kuishiwa nguvu, vidonda vya koo, vipele vya ngozi, maumivu ya tumbo, kuharisha (damu), kutapika damu na kutokwa damu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.