RAS Mwanza awaahidi JWTZ Ushirikiano kwenye Miradi Mkoani humo
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana ameliahidi Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ) kushirikiana nao kwenye Miradi mbalimbali ya kimkakati iliyopo mkoani humo ili iimarike kiulinzi na kiusalama kwa tija ya wananchi.
Mtendaji huyo wa Mkoa amezungumza hayo mapema leo Disemba 29, 2023 Ofisini kwake wakati wa mazungumzo mafupi na Meja Generali Shaaban Mani ambaye ni mkuu wa kamandi ya anga kutoka JWTZ, amesema kutokana na Teknolojia inavyozidi kushika kasi jeshi hilo lina umuhimu mkubwa kuhusishwa kwenye miradi hiyo ili nalo lijipange vizuri katika kutekeleza majukumu yake.
"Tuliona mwaka 1978 wakati wa vita dhidi ya Idd Amin Daraja la mto Kagera lilivyo shambuliwa na adui,hilo ni somo kwetu vikosi vya jeshi kuwa karibu na miundombinu kama hiyo," amefafanua Balandya wakati akizungumza na mgeni wake.
Balandya amebainisha Mwanza ina miradi mingi inayoendelea kujengewa kuanzia Reli ya kisasa,SGR,Daraja la JP Magufuli na Meli ya abiria Mv Mwanza na kituo cha kimataifa cha ulinzi na uokoaji Ziwa Victoria kilichopo mbioni kujengwa cha Jumuiya ya Afrika Mashariki ambacho makao makuu yake yatakuwa Mwanza,miradi yote hiyo watashirikiana na Jeshi ili izidi kuwa endelevu
"Sisi kama Jeshi ni wajibu wetu kuhakikisha muda wote Taifa lipo salama,nimefika Mwanza ili kukagua miundombinu yetu iliyopo chini ya kikosi cha anga na kama kuna changamoto ni kuzifanyia kazi haraka,"Mej Gen.Mani.
Katika mazungumzo hayo Mkuu huyo wa kikosi cha anga amemuomba Katibu Tawala wa Mkoa kuwapa maeneo yaliyovamiwa na wananchi ili waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
"Maeneo ya Jeshi ni lazima yawe mbali na makazi ya wananchi,kitendo cha nyumba za raia kuwa karibu yetu ni hatari pia kwa usalama wa nchi kwa mtu atakaye kuwa na nia mbaya,"amesisitiza Mej.Gen.Mani
Wakati huo huo Ndg.Balandya Elikana amemkaribisha rasmi Mkuu mpya wa Uhamiaji Mkoa wa Mwanza,Kamishna msaidizi,Kola Kayumba anayechukua nafasi ya mtangulizi wake Kamishna msaidizi Peter Mbaku anayehamia Mkoa wa Rukwa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.