Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana amewataka Maafisa Biashara na Afya ngazi ya Wilaya hadi Mkoa kuzingatia mafunzo wanayopatiwa kuhusiana na udhibiti wa ubora na usalama wa chakula na vipodozi ili wananchi waendelee kupata bidhaa bora na kukuza Uchumi wa nchi.
Akifungua Mafunzo ya siku moja Mkoani Mwanza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa yaliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania TBS kwa kushirikiana na TAMISEMI Katibu Tawala Msaidizi Utumishi na Rasilimali watu Daniel Machunda amesema Serikali imeamua kuwatumia Watumishi ili kulinda afya za wananchi katika maeneo yao.
"Niwapongeze sana TBS na TAMISEMI kwa kubuni mpango huu ambao utawawezesha Watumishi hawa kufanya kazi zao kwa weledi na kuzingatia Sheria na miongozo iliyopo hasa kwa kuzingatia wingi wa bidhaa kutoka ndani na nje ya nchi ambazo baadhi siyo salama kwa matumizi," amesema Machunda.
Amewataka watumishi hao wanayopatiwa mafunzo wasiyatumie kwenda kutumia nguvu kwa watakaobainika wamekwenda kinyume badala yake watumie sheria, miongozo na maadili.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu kutoka TBS Makao Makuu Lazaro Henry amebainisha kuwa mpango huo umekuja kwa kutambua soko la ushindani wa biashara ulivyo hivi sasa, hivyo Watumishi hao watakuwa chachu ya ushauri kwa viwanda nchini lengo viendelee kutoa bidhaa bora kwa mlaji na mtumiaji.
Shirika la Viwango Tanzania TBS lina majukumu makuu manne ambayo ni Kuweka Viwango vya Kitaifa vya bidhaa, huduma na mifumo ya usimamizi wa ubora katika Sekta zote pamoja na kutekeleza Viwango vya Kitaifa katika Sekta za viwanda,biashara na huduma kwa kutumia skimu mbalimbali za udhibiti ubora.
Zingine ni pamoja na Upimaji wa bidhaa kwa lengo la kuhakikisha ubora wake na kutoa mafunzo Kwa wazalishaji pamoja na wafanyakazi kutoka Taasisi na Viwanda.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.