RAS Mwanza awashauri Wataalamu wa Tiba asili na Tiba mbadala kujiendeleza kielimu ili kutoa huduma bora kwa wananchi
Kaimu Katibu Tawala Mkoa Mwanza Chagu Nghoma amewashauri Wataalamu wa Tiba asili na Tiba Mbadala kuchangamkia fursa za kujiendeleza kielimu ili kujiaminisha katika kutoa huduma zao,
Akizungumza leo Oktoba 14, 2023 kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika hafla fupi ya kuwakabidhi vyeti vya kuhitimu mafunzo, Chagu amesema bado asilimia kubwa ya Watanzania wanatumia tiba zao hivyo ni wajibu wao kuhakikisha huduma zao zinazingatia miongozo sahihi kutoka Wizara ya afya.
"Naipongeza Wizara ya Afya kwa kutoa mitaala ambayo mmefundishwa,hii itawasaidia kutoa huduma zenu vizuri na kujenga Imani zaidi kwa wananchi," Nghoma.
Amesema huduma za Tiba asili zimekuwa zikitumika kwa miaka mingi hapa nchini tangu enzi za mababu zetu, lakini Serikali kwa kutambua unyeti wa huduma zenu imeona ni vizuri ziboreshwe kwa kupatiwa mafunzo kama haya.
"Haiwezekani ukatoa huduma kwa mgonjwa bila kwanza kujua anaumwa nini,ni lazima upate vipimo vyake ili ufahamu kiini cha tatizo lake na kuanza kumhudumia,"amesisitiza Nghoma wagonjwa kupata vipimo sahihi kabla ya kupatiwa Tiba mbadala.
Kuhusu wataalamu wa Tiba asili wanaoibuka kila uchao na kujitangaza ni mabingwa wa magonjwa mbalimbali amewataka kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara ya afya kwani baadhi yao wamechangia vifo kwa wananchi kwa upotoshaji.
"Chuo chetu cha Mwanza Polytechnic kimeanza kutoa mafunzo haya kwa mara ya kwanza,na tunatarajia kutoa mafunzo zaidi kwani Mkoa wa Mwanza una wataalamu wa Tiba asili na mbadala zaidi ya elfu mbili,hivyo mafunzo kama haya ni muhimu kwao",Jerry Nyabululu,Mkurugenzi wa Chuo.
Awali akitoa taarifa ya malengo ya mafunzo hayo kwa mgeni rasmi,mratibu wa mafunzo Dkt.Sally Giyunga amebainisha Wataalamu hao wamefundishwa namna ya kuandaa dawa mbadala,Sheria ya Tiba asili na mbadala,ukusanyaji wa dawa ghafi na namna ya kuzikausha kupitia nishati ya jua pamoja na namna ya huduma magonjwa yasiyoambukiza na yanayoambukiza.
"Tumekuwa na Moduli 13 kutoka Wizara ya afya na tulikuwa wakufunzi 3 tuliotoa mafunzo haya kwa wataalamu hawa wapatao 90,"Dkt.Giyunga
"Ndugu mgeni rasmi tunaishukuru Wizara ya afya kwa kuona umuhimu wa sisi kupatiwa mafunzo haya,ombi.letu tunaomba kupunguziwa gharama za vipimo kwa wateja wetu ili tuweze kutoa huduma bora",Kawawa Athumani,Katibu wa Chama cha wataalamu wa Tiba asili Mwanza(CHAWATIATA)
Kauli mbiu ya Wahitimu hao inasema "Waganga kwa afya bora ya Watanzania".
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.