RAS MWANZA AWATAKA VIJANA KUTUMIA MATOKEO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI KUJIINUA KIUCHUMI
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Chagu Nghoma amewataka Vijana mkoani humo kutumia Takwimu za matokeo ya Sensa ya watu na Makazi ya mwezi Agosti 2022 kujikita kwenye Sekta zenye tija ili kujiimarisha na kujiinua kiuchumi.
Ametoa rai hiyo leo Oktoba 16, 2023 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi yaliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa Vijana Mkoani humo chini ya Uratibu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Amesema, vijana ndio kundi linalotegemewa kuchagiza uchumi wa nchi kwa sasa na siku za baadae hivyo ni lazima wawe na taarifa sahihi za eneo gani lina tija endapo watajihusisha nalo mathalani biashara, kilimo au uvuvi na kwamba majibu ya suala hilo yanapatikana kwenye takwimu zilizokusanywa wakati wa Sensa.
"Suala la ajira ndilo eneo lenye changamoto zaidi kwa vijana wa Mwanza, hivyo tunaishukuru sana Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuwapa mafunzo kundi hilo kwani wataweza kutumia takwimu hizo kuona sehemu gani ina fursa ya kujiinua kiuchumi endapo watajikita nayo." Amefafanua.
Aidha, ametumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia kwa kuweka fedha nyingi kwenye miradi ya kuwainua vijana kiuchumi kama ujenzi wa kesho bora kwenye kilimo na mifugo (BBT) ambapo ametolea mfano shamba la Taifa la Mifugo la Mabuki ambapo vijana wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya ufugaji wa kisasa na wakifikisha ujuzi huo kwa wengine watasaidia kuboresha sekta hiyo.
Ndugu Nghoma ametaja pia mikopo inayotolewa kwa ajili ya kufanya ufugaji wa kisasa kwa njia ya vizimba na ufadhili wa vijana kwenye mafunzo ya uanagenzi kupitia vyuo vya Ufundi stadi nchini (VETA) kuwa ni miongoni mwa maeneo yenye fursa ya kupata ujuzi na kusaidia kujikita kwenye uzalishaji wenye tija.
Mdoka Omary, Mtakwimu mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu amesema kuwa mafunzo hayo ni katika utekelezaji wa muongozo uliozinduliwa na Rais Samia wa kuhakikisha matokeo hayo yanasambazwa katika ngazi zote ili takwimu hizo zifike hadi vijijini.
Amefafanua kuwa matokeo ya Sensa ya watu na Makazi yanatoa majibu na fursa ya eneo gani liongezewe nguvu katika suala la utegemezi ambao imefikia 87 asilimia kwa kila watu 100 wa umri wa kufanya kazi na Mwanza imefikia zaidi ya asilimia 100 hivyo inatoa fursa kwa vijana kujikita kwenye uzalishaji ili kutoka kwenye uzalishaji.
Mkoa wa Mwanza unashika nafasi ya pili kwa idadi kubwa ya watu nchini ukitanguliwa na Mkoa wa Dar es salaam kwa kuwa na idadi ya watu Milioni 3.7 huku ikiwa na Kaya Laki Saba ambapo Jiji la Mwanza likishika nafasi ya kwanza kwa kuwa na watu Laki Tano huku Ukerewe ikiwa na watu wachache zaidi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.