Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ngusa Samike amewataka Wataalamu wa Afya kutoka Halmashauri zote Mkoani humo kuleta Mageuzi chanya kwenye Sekta hiyo hasa suala zima la Afya ya mama na mtoto.
Akifungua Kikao kazi cha Wataalamu hao cha Wilayani Sengerema walichokutana kujadili changamoto na kupanga mbinu bora za kuboresha afya ya mama na mtoto, Samike amesema bado kunahitajika uwajibikaji wenye Weledi katika kuboresha huduma ya afya kwa ujumla.
"Kila mwaka mnakuwa na vikao vya namna hii kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo lakini nikiangalia takwimu za mabadiliko hayaridhishi hasa suala la vifo vya mama na mtoto, anzeni kubadilika" amesisitiza Katibu Tawala.
Amewakumbusha Waganga Wakuu wa Wilaya kutumia muda mwingi kuzungukia kwenye Vituo vya Afya na kuzitatua changamoto zilizopo kwani kwa kufanya hivyo kutaongeza ari ya uwajibikaji kwa Watumishi wengine.
Ndugu Samike ameishukuru pia Serikali ya awamu ya Sita kwa kuendelea kujenga ushirikiano mzuri na Taasisi zisizo za Kiserikali ambazo zimekuwa zikitoa mchango katika Miradi mingi ya afya Mkoani Mwanza.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa amesema atasimamia na kutekeleza maagizo yote yanayolenga kutatua changamoto katika Sekta ya afya mkoani humo.
Kikao hicho cha siku 3 cha kupanga mfumo wa Afya ya uzazi kinaratibiwa na Shirika la USAID AFYA YANGU huku kikiwajumuisha watalaamu wa afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa, Waganga Wakuu wa Wilaya na Waratibu wa afya kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.