RAS MWANZA AZINDUA RASMI KAMBI YA MADAKTARI BINGWA BOBEZI HOSPITALI YA SEKOU TOURE
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana amezindua rasmi kambi ya siku tano ya Madaktari bingwa bobezi wa moyo na huduma ya tiba kwenye hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Mwanza-Sekou Toure na kuwahimiza wananchi wote kuchangamkia fursa hiyo ya matibabu.
Akizungumza leo Oktoba 28, 2024 na wananchi waliofika kwenye uzinduzi huo uliofanyika hospitalini hapo, Balandya amesema bado takwimu zinaonesha magonjwa yasiyoambukiza yanazidi kuongezeka ukiwemo shinikizo la damu ambao umeshika nafasi ya kwanza miongoni mwa magonjwa kumi.
"Zoezi hili ni muhimu sana kwetu sisi na tuzidi kupeleka taarifa kwa wananchi ili wafike kwa wingi kupata matibabu na ushauri pia, tusisubiri hadi hali iwe mbaya ni vizuri kujiangalia afya zetu mapema na kuanza matibabu," amesisitiza mtendaji huyo wa Mkoa.
Aidha, ameishukuru Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwaleta wataalamu hao na kutoa huduma hiyo Ijulikanayo kama "Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan Outreach Service" ambayo inasaidia kuimarisha afya za wananchi na hasa kwa kipindi hichi ambapo magonjwa yasiyoambukiza yanavyozidi kushika kasi.
Balandya pia ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuonesha kwa vitendo mkakati wa kuiboresha hospitali ya Sekou Toure ambayo inawahudumia wananchi zaidi ya milioni 3.
"Kambi hii ya siku tano tunatarajia kuleta matokeo chanya kwa wananchi wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo na mengineyo na hasa ambao wanaishi pasipo kujielewa changamoto zao za afya". Dkt.Jessica Lebba, Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Sekou Toure, Bahati Msaki amebainisha kambi hiyo imeanza leo hadi Novemba Mosi mwaka huu na baada ya hapo matibabu kama hayo yataendelea hospitalini hapo kwani wapo madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali yakiwemo yasiyoambukiza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.