RAS MWANZA AZITAKA NGOs KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUONDOA WATOTO WA MTAANI
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Balandya Elikana ameyataka Mashirika yasiyo ya Serikali Mkoani humo kushirikiana na Serikali kuwaondoa watoto wa mtaani kwa kuwapa elimu na kuwawezesha kubadili mtazamo wa maisha.
Ametoa wito huo leo tarehe 27 Januari, 2025 wakati akifungua Mkutano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali zaidi ya 600 yanayofanya kazi mkoani humo yaliyoketi kwa utambulisho na kuwasilisha hali ya utekelezaji wa shughuli zao.
"Inawekezana pamoja na sababu zingine watoto wa mtaani wanasababishwa pia na ongezeko la watu kwani Mwanza ina muingiliano mkubwa wa watu hadi kufikia idadi ya milioni 3.6 hadi 4, hivyo tunapaswa kuhakikisha tunaitumia ardhi vizuri." Amesema Balandya.
Ameongeza kuwa, sekta ya uvuvi ina fursa nyingi za kuinua kiuchumi jamii mathalani ufugaji wa samaki kwa njia ya kisasa ya vizimba hivyo NGOs zihusishe jamii katika kuchakata chakula, kuzalisha vifaranga na hatimaye kuwa na ufugaji wa kisasa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Bi. Mwamtumu Mahiza, amesema kuwa Serikali inachukua juhudi za makusudi kutambua changamoto za wadau hao ili kuwasaidia waweze kukidhi vigezo vya kusajiliwa na kuenenda vyema katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu ya sheria.
"Kwenye orodha nikiletewa taarifa nakuta mashirika zaidi ya elfu 10 lakini kwenye mfumo hawafiki elfu 4 na kwa hapa Mwanza ni miongoni mwa sehemu yenye shida hiyo maana naambiwa kuna mashirika zaidi ya 654 lakini 116 tu ndio wanalipa ada, tujirekebishe jamani." Bi. Mahiza.
Ameongeza kuwa NGOs hususani zinazojihusisha na Afya zinapaswa kufanya kazi kwa uzalendo kwa kulinda utamaduni, silka na utu wa nchi na sio kutoa taarifa za uongo ili kupata fedha za ufadhili mathalani kwenye taarifa za maambukizi na milipuko ya magonjwa nchini.
"Sisi NGOs bado tuna shida pamoja na kuwezeshwa na Serikali bado kiwango cha kuwajibika kwa mujibu wa sheria kiko chini kama vile usajiri na kulipa ada za uanachama kila mwaka na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria hatuko vizuri ni lazima tujirekebishe." Amesema Gaspar Makala, Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali ..
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.