Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima ametoa siku 20 kwa Mafundi wanaojenga Kituo cha Afya cha Maisome kukamilisha Ujenzi wa Majengo ya Mapokezi ya wagonjwa OPD na Maabadara ili huduma za afya zianze kutolewa.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo mapema leo kwenye Kisiwa hicho kilichopo kata ya Maisome-Buchosa wilayani Sengerema alipofika kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa kituo hicho pamoja na nyumba ya watumishi ambavyo Mwaka 2021 walipokea jumla ya Shilingi Milioni 250 kutoka Serikali kuu kupitia chanzo cha Tozo za Miamala ya Simu.
Amesema, kisiwa hicho chenye zaidi ya wananchi Elfu Ishirini kinapaswa kupata huduma za Afya zilizokamilika kwani wananchi wako mbali na maeneo mengine yenye huduma za Afya na hilo ndio lengo la Serikali kuleta fedha hizo lakini usimamizi umekua dhaifu na kusababisha ucheleweshaji.
"Wananchi zaidi ya Elfu Ishirini wa kisiwa hichi (Maisome) wamecheleweshwa kupata huda za Afya kwa zaidi ya Mwaka mmoja kutokana na usimamizi dhaifu kwenye Ujenzi huu, sasa nawapa siku 20 kufukia tarehe 19 Machi, 2023 muwe mmemaliza kujenga ili huduma zitolewe" Amesema Malima.
Katika hatua ingine, Mkuu wa Mkoa amewaagiza TAKUKURU kuupitia mradi huo ili ilikujiridhisha ni kwanini fedha zilizotengwa kujenga Kituo hicho hazikutosha hadi Halmashauri kuongeza Shilingi Milioni 30 kutoka mapato ya ndani na bado kuna malalamiko ya madai kwa mafundi wanaojenga mradi huo.
Vilevile, Mhe Malima ameitembelea shule pekee ya Sekondari kisiwani humo iitwayo Maisome na katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujifunza ametoa ahadi ya kuwajengea Mabweni mawili kwenye shule hiyo ili kuwapunguzia umbali wa zaidi ya Kilomita 12 wanafunzi wanaotoka vijiji vya mbali kama Busikimbi.
Akizungumza kwenye mkutano wa wananchi we kero, kiongozi huyo amemuagiza Mzabuni anayetoa huduma ya nishati ya umeme kisiwani humo kupunguza gharama za kila Uniti Moja utoka 3500 ili wananchi waweze kumudu na vilevile waongeze uwezo wa huduma uendane na mahitaji.
Mhe. Erick Shigongo, Mbunge wa Jimbo la Buchosa ameahidi wananchi kutatua changamoto kadhaa zinazowakabili wananchi wake kama kuboresha huduma ya Maji kwani tayari Rais Samia ameshawakabidhi Milioni 280 za kujenga miradi ya Maji na pamoja na ujenzi wa Barabara kuu ya kuongia jimboni humo kwa kiwango cha Changarawe.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe. Senyi Ngaga amemshukuru Rais Samia kwa kuwahudumia wananchi kwa kuwapatia fedha za kutekeleza miradi mbalimbali na amemuahidi Mkuu wa Mkoa kutekeleza maagizo aliyoyatoa kwenye ziara yake aliyoifanya katika kuhakikisha wananchi wanaboreshewa mazingira
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.