Leo Juni 29, 2022 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amekabidhi Pikipiki 13 zenye thamani ya Milioni 42.1 kwa Mameneja wa RUWASA Wilaya pamoja na kwa Vyombo vya Watoa huduma za Maji ngazi ya jamii (CBWSOs).
Akizungumza na wafanyakazi, wadau wa Maji na wananchi, Mkuu wa mkoa ametoa rai kwa RUWASA kukusanya Maduhuli ya Maji na kuhakikisha wanawafikia wateja kwa haraka na kutatua kero zao huku akibainisha kuwa kwa kufanya hivyo taasisi hiyo itasimamia vema Skimu na Miradi ya Maji na watatoa huduma bora kwa wananchi.
"Vyombo hivi lazima tuvitunze na kuhakikisha vinatumika kwa malengo kusudiwa pekee na Meneja RUWASA hakikisha zile Pikipiki 8 Mbovu zinakarabatiwa ili kukamilisha pikipiki 30 zinazotoa huduma kwenye uimarishaji wa huduma katika miradi yetu ya maji." Mhe Gabrie.
Aidha, ameagiza kuondolewa wakandarasi wanaokwamisha miradi ya maji ili dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama Ndoo iweze kutimia kwa upatikanaji wa Maji kwa urahisi kwenye jamii na ameahidi kuwa mkoa utafuatilia wabadhirifu watakaolenga kuhujumu miradi ya maji na watachukuliwa hatua.
Mhandisi Daud Amlima, Kaimu Meneja RUWASA Mkoa ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maji kwa kuwaletea vitendea kazi hivyo na amebainishaa kuwa pikipiki hizo zitakua Msaada mkubwa katika kuimarisha Miradi na skimu za Maji vijijini.
"Katika mwaka 2021/22 RUWASA Mkoa wa Mwanza imesaini Mikataba 51 yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 83 itakayohudumia zaidi ya watu 560,000 sawa na Asilimia 20 ya wananchi wanaoishi Vijiji, miradi hii itakapokamilika itafanya huduma za maji Vijijini kufikia asilimia 88" Mhandisi Amlima amefafanua.
Naye, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mwanza Mhe Ellen Bogohe, ameishukuru serikali kwa kuwa bega kwa bega na wananchi na kwamba uwepo wa pikipiki hizo umeitendea haki Ibara ya 100 ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwani zitaboresha Maisha ya wananchi Vijijini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.