Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel amewapongeza na kuwashukuru watumishi wa Ofisi yake kwa ushirikiano uliozaa ufanisi mkubwa kwenye kazi kwa kipindi cha mwaka wa fedha ulioishia juni 30, 2022.
Amebainisha hayo kwa furaha mchana wa leo Julai 1, 2022 katika kikao cha kufungua Mwaka mpya wa fedha 2022/23 kilichowakutanisha watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili kufanya tathmini ya kazi zilizotekelezwa katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita.
"Hongereni kwa kazi nzuri mliyofanya mwaka ulioisha, Mwaka huu Mpya tuna deni kubwa katika kuwahudumia wananchi kupitia ofisi zetu hivyo pamoja na tathmini tunayoenda kufanya ni wajibu wetu kuongeza ushirikiano na kuombeana kheri katika kazi." Mkuu wa Mkoa.
Vilevile, amewakumbusha watumishi wa Ofisi hiyo kuzingatia Melengo ya Makusanyo yaliyo mbeleni na amewataka kuketi na wataalamu wanaohusika na makusanyo katika halmashauri zote ili kuangalia kwa pamoja ni viashiria vipi vya makusanyo vinaonesha kuleta tija.
"Kwangu mimi siwaoni nyie kama wafanyakazi wenzangu bali nawaona kama ndugu zangu, ndani ya mwaka huu tumefanya makubwa nami naongeza maombi ili tuwe na afya njema na tuzidi kuwa bora katika kazi." Mkuu wa Mkoa amesema.
"Hivi karibuni nimezunguka kwenye Halmashauri zote za Mkoa huu kwenye Vikao vya Mabaraza ya CAG na nimeona changamoto kadhaa na tunahitajika sana katika kuwasaidia hasa kuepuka matumizi mabaya ya fedha ili kuepuka hoja." Amesema, Mhe. Gabriel.
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa Ngusa Samike amemshukuru Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Ofisi hiyo zaidi ya Tshs Bilioni 1 ambazo zinatekeleza maboresho ya Miundombinu pamoja na ujenzi wa Nyumba za Makatibu Tawala Wasaidizi, Ukarabati wa Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Ujenzi wa Ofisi za Maafisa Tarafa.
"Ndugu watumishi wenzangu, tumekutana hapa leo kufanya tathmini ya tulikotoka na kuweka mikakati mipya kwa mwaka wa fedha tunaouanza katika kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na kuboresha mazingira ya kazi." Amesema Samike.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.