RC MAKALLA AAGIZA KUANZA MARA MOJA KWA UJENZI WA BARABARA YA SENGEREMA-BUCHOSA
*Awataka TANROADS kumpatia Mkandarasi maeneo yasiyo na mgogoro waanze kujenga mara moja*
*Aiagiza Halmashauri ya Sengerema kuhakiki madai ya wananchi wenye Ofa na Hati kwenye mradi huo*
*Aitaka Halmashauri kuweka vipaumbele kwenye Mapato ili kuwe na mpango wa ulipaji wa madeni mbalimbali*
*Aagiza utatuzi wa migogoro kwa haraka ili kudhibiti uvunjifu wa amani kwenye familia*
*Awataka watendaji ngazi za Kata na Vijiji kutenga siku kwenye wiki kusikiliza kero hususani za ardhi na kuzimaliza*
*Auagiza uongozi wa Wilaya na Halmashauri kutathmini Madai ya fidia kwenye ujenzi wa stendi*
*Ataka kutekelezwa kwa maagizo yote aliyoagiza ndani ya siku 14 na apate taarifa ya utekelezaji wake*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe CPA Amos Makalla amemtaka Mkandarasi AVM-Dilingham anayejenga barabara ya Sengerema- Buchosa yenye urefu wa Kilomita 54.4 kwa gharama ya zaidi ya Bilioni 73 kuanza mara moja ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa mujibu wa Mkataba.
Ametoa agizo hilo leo Novemba 08, 2023 wakati wa usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi kwenye mkutano uliofanyika kwa zaidi ya saa 11 kwenye Stendi ya zamani ya Mabasi Sengerema na kubaini kuwa tangia mkataba usainiwe mwezi Aprili ujenzi haujaanza huku zikitajwa sababu mbalimbali.
Mhe. Makalla amesema haiwezekani mkataba wa ujenzi wa mradi huo usainiwe mwezi aprili lakini hadi sasa ujenzi wake usianze tena kwa sababu za kizembe wakati Mhe. Rais ameridhia kujengwa kwa barabara hiyo na fedha ameshatoa.
"Ninawaagiza TANROADS mhakikishe mkandarasi anaanza ujenzi wa hii barabara mara moja hususani kwenye maeneo ambayo hayahitaji kufidia ardhi, Serikali imeridhia kujenga barabara hii sasa kwanini tunachelewa ujenzi huu ambao wananchi wameisubiri kwa muda mrefu." Makalla amesisitiza.
Aidha CPA Makalla ameitaka halmashauri ya Sengerema kuhakiki madai ya wananchi wanaodai kuchukuliwa maeneo yao kupisha ujenzi huo ili ibainike nani ana ofa au Hati na uhalali wake ili gharama stahiki zifahamike na kulipwa mara moja na ujenzi uendelee.
"Wakati tunashughulikia eneo lenye mgogoro nawaagiza Halmashauri ihakiki eneo lenye ofa au Hati za kisheria ili tujue gharama na mniletee taarifa ili tutangaze kuwa eneo fulani lina mgogoro kutokana na wananchi kupewa Hati kwenye eneo la barabara", Mkuu wa Mkoa.
Kutokana na kukithiri kwa kero za ardhi, Makalla amewaagiza watendaji kuanzia ngazi za vijiji na Kata kutenga siku maalum ndani ya juma kusikiliza na kutatua kero za wananchi ili kuwajengea Imani na Serikali ya Rais Samia ambayo imejipambanua kwenye kuhudumia wananchi wakati wote.
"Punguzeni matatizo na kero za ardhi kwa wakati kwani kuongezeka kwa kero kwenye eneo fulani sio sifa nzuri hususani kwenye sekta moja, hapa leo zaidi ya asilimia 90 ya kero zilizowasilishwa ni za ardhi sasa maana yake ni kwamba idara hii na watendaji hawafanyi kazi zao vizuri na lazima tujirekebishe kwa kusikiliza kero za wananchi." Makalla.
Vilevile, Mhe. Mkuu wa Mkoa ameutaka uongozi wa Wilaya na wataalamu wa ardhi wafike kwenye eneo lenye wadai 29 wa fidia waliopisha ujenzi wa kituo cha Mabasi cha wilaya hiyo kufanya tathmini na kamati ya fedha ijulishwe madai halali na yalipwe ili kuondoa kero hiyo inayowakabili wananchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.