RC MAKALLA AAGIZA TANESCO NA RUWASA KUPELEKA HUDUMA ZA MAJI NA UMEME KWENYE UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA MWANZA
*Awapongeza Magu kwa Usimamizi mzuri wa Ujenzi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Magu kwa Usimamizi mzuri wa Mradi na amewaagiza TANESCO na RUWASA kupeleka huduma za Umeme na Maji kwenye Shule ya Sekondari ya wasichana ya Mwanza (Mwanza Girls) inayokamilishwa kujengwa.
Mhe. Makalla ametoa agizo hilo mapema leo jumanne Julai 11, 2033 wakati alipofanya ziara kwenye kijiji cha Ihushi-Bujashi kwa ajili ya kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari ya Wasichana Mwanza (Mwanza Girls) inayotekelezwa kwa zaidi ya Bilioni 3 fedha kutoka kutoka Serikali kuu.
"Mtu wa Maji na Umeme pokeeni kilichopo na utaendelea kudai fedha zingine ili wanafunzi hawa wapate maji au umeme, hizi ni huduma muhimu sana hivyo hatuwezi kuzikosa nataka muanze mpango kazi wa kutekeleza kwa haraka nawe wa barabara tengeneza kwa haraka kwa kutumia kile kidogo kilichopo." Mhe. Makalla.
"Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kuweka alama hii na mabadiliko makubwa kwenye Sekta ya Elimu wilaya kwetu na Mkoa kwa ujumla, nasi tunamwombea kheri kwa Mwenyezi Mungu na tunamtia moyo aendelee kuwainua watoto wa kike wa nchi hii." amesema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mhe. Simon Mpandalume.
Akitoa taarifa ya Utekelezaji wa Ujenzi wa Shule ya Wasichana ya Mwanza (Mwanza Girls), Afisa Elimu Sekondari ya Magu, Beatrice Balige amesema kuwa Halmashauri hiyo imepokea Shilingi bilioni 3 kati ya nne zilizotengwa na kwamba utekelezaji kwa ujumla umefikia zaidi ya asilimia 90 na kwamba wamejiwekea mikakati madhubuti ya kukamilisha kwa wakati.
Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo imepokea zaidi ya bilioni Moja kwa ajili ya Ujenzi wa Miundombinu mingine na kwamba Shule hiyo kwa sasa ina Changamoto ya chanzo imara cha Maji pamoja na Umeme na kutokana na ufinyu wa bajeti kwenye eneo hilo huku akibainisha kuwa shule hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.