RC MAKALLA AELEZA MKAKATI WA KUFANYA UWANJA WA NDEGE MWANZA KUWA WA KIMATAIFA
*Aagiza Mamlaka ya Uwanja wa Ndege kuandaa michoro ya jengo la Abiria, Upanuzi,Hoteli na Shopping Mall*
*Fedha Bilioni 11 zipo tayari kuanzia uboreshaji*
*Aeleza mikakati ya kuwaondoa wavamizi wa uwanja ndege*
*Uwepo wa wavamizi ni hatari kwa usalama wao na Ndege*
Mhe. CPA Amos Makalla, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amesema Serikali ina mkakakati wa kuufanya uwanja wa Ndege wa Mwanza kuwa wa Kimataifa kwa kujenga Miundombinu ya kisasa likiwemo jengo la abiria ambapo amebainisha kuwa tayari zaidi ya Bilioni 11 zipo kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi huo.
Amebainisha hayo mapema leo tarehe 13 Septemba, 2023 wakati wa kikao na watumishi wa Uwanja wa Ndege Mwanza ambapo ameagiza pia Mamlaka ya Uwanja wa Ndege kuandaa michoro ya jengo la abiria, upanuzi, Hoteli na Shopping Mall ili kuleta unadhifu kwenye huduma.
Katika uboreshaji huo CPA Makalla amewataka Mamlaka ya viwanja vya ndege kuendelea na shughuli mbalimbali kama ujenzi wa Jengo la abiria la kisasa huku akibainisha kuwa hawapaswi kusubiri tena kwani limekua likichelewa kujengwa na Serikali ya Rais Samia imeamua kuboresha uwanja huo kuwa wa kimataifa.
"Nilikuja hapa nikiwa na siku tatu tu Mwanza na nlielekeza muanze ujenzi mara moja tena kwa bahati mna fedha za kuanzia tena ni Bilioni 11 na kazi ya kwanza mliyotakiwa kuanza nayo ni kusanifu namna bora ya ujenzi wa Jengo ambalo litakua la kimataifa kwa ajili ya kuubadilisha uwanja wetu kuwa wa kimataifa." Mkuu wa Mkoa.
CPA Makalla amesema shughuli za mamlaka ya viwanja vya ndege pamoja na jeshi la anga kwenye eneo hilo hazipaswi kuingiliwa na wananchi waliovamia na kwamba Serikali ipo kwenye uboreshaji wa uwanja huo kuwa wa kimataifa ndio maana kuna shughuli mbalimbali zinaendelea.
Mhe. Mkuu wa Mkoa amefafanua kuwa Serikali inaandaa utaratibu wa kuwaondoa wananchi zaidi ya Elfu Moja (Nyumba 800) wa Mitaa ya Mhonze, Kihili na Bukyanhulu waliovamia eneo la Mamlaka ya Uwanja wa ndege ili kutoa fursa kwa shughuli za Uwanja kufanyika katika hali ya usalama.
"Kwakua Mwanza tunaanza safari ya kuubadilisha uwanja wa ndege kuwa uwanja wa kimataifa, Mamlaka inahitaji eneo lote na kwa ajili ya usalama pia maana jeshi la anga wanalihitaji eneo hilo pia kwa usalama wa ndege zao, za abiria na kwa usalama wa wananchi wetu pia." CPA Makalla.
Meneja wa Uwanja wa Ndege Mwanza, Ndugu Mussa Mcholla amebainisha kuwa katika kuweka mazingira bora wa usafiri wa anga nchini Serikali imefanya maboresho ya kimkakati yaliyohusisha urefushaji wa barabara ya kutua na kuruka ndege, ujenzi wa Jango jipya la abiria na Miundombinu mingine.
"Serikali imefanya maboresho ya kimkakati kama urefushaji wa wa barabara ya kutua na kupaa, upanuzi na ujenzi wa tabaka la mwisho la lami pamoja na ujenzi wa jengo jipya la mizigo na barabara za maungio ya ndani kwa ajili ya magari na mfumo wa maji taka." Amesema Meneja.
Awali ndugu Mcholla aliwasilisha ombi rasmi kwa Mkuu wa Mkoa la kusaidia kutatua migogoro ya ardhi kwenye eneo la uwanja huo kutokana na uvamizi uliofanywa na wananchi wanaoishi kwenye mitaa ya Mhonze, Kihili na Bukyanhulu.
"Mhe. Mkuu wa Mko hapa kuna mgogoro wa ardhi ambapo wananchi wamevamia eneo la uwanja wa ndege tena wapo katikati ya eneo la jeshi upande wa chini na juu ambapo kiusalama inakua changamoto sana maana kuna operesheni za kiraia na za kijeshi kwenye eneo hili ikiwepo mazoezi na siku ikianguka ndege maafa yatakua makubwa sana." Meneja Uwanja wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.