RC MAKALLA AMTAMBULISHA RASMI KOCHA MKUU WA PAMBA JIJI FC, MBWANA MAKATTA
*Atambulisha jina jipya la timu kuwa ni Pamba Jiji Football Club*
*Asema timu imempata kocha mwenye viwango na uzoefu wa mechi za Ligi kuu*
*Awaomba wana Mwanza kuunganisha nguvu zao ili timu ipande Ligi kuu msimu ujao*
Hatimaye timu ya soka ya Pamba Jiji FC ya Mkoani Mwanza inayoshiriki Ligi ya Championship imempata kocha Mkuu mpya Mbwana Makatta akisaidiana na msaidizi wake, Renatus Shija aliyeingia kandarasi ya mwaka mmoja ya kuinoa timu hiyo maarufu kama TP LINDANDA.
Akimtambulisha leo mbele ya vyombo vya Habari kwenye ukumbi mkubwa wa Ofisi yake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla ambaye ni mlezi wa timu hiyo amebainisha baada ya kufanya mchakato wa kina hatimaye wamempata mtaalamu huyo wa ufundi wa uhakika.
"Namtambulisha kwenu kocha mpya Mbwana Makatta, hapa nawahakikishieni hatukubahatisha kumpata,namfahanu vyema uwezo wake na nina imani tutafika malengo yetu ya kucheza Ligi kuu msimu ujao,"CPA Makalla.
Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ni mkereketwa wa michezo amesema baada ya kuimarisha dawati hilo la ufundi, kinachofuata sasa ni maandalizi ya timu kuingia kambini Agosti Mosi 2023 huku mtaalamu huyo wa ufundi akiendelea kuipitia ripoti ya mtangulizi wake na yeye kutoa mapendekezo yake baada ya kuwaona wachezaji uwezo wao.
"Kocha nikuondoe shaka tuna kasumba baadhi yetu kuwa na orodha ya nani umpange nani umwache katika mchezo husika,hilo la kuingiliwa hapa hutaliona na badala yake uamuzi wa mwisho utabaki kwako hata kama mimi nina mahaba na mchezaji fulani hilo lisikukwaze",amesisitiza mlezi wa timu hiyo.
"Nashukuru kwa wamiliki wa timu hii ambao ni Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kuniamini kushika nafasi hii,nina wahaidi sitowaangusha katika kufikia malengo ya kucheza Ligi kuu msimu ujao,"Mbwana Makatta,Kocha Pamba Jiji FC
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza ambao ndiyo wamiliki wa timu hiyo,Aaron Karugumjuli amebainisha kazi iliyo mbele yao ni kumpa ushirikiano kocha huyo ili kukata kiu ya wana Mwanza ya kuona timu yao ikishiriki Ligi kuu.
"Kocha Mbwana ni mzoefu na amefundisha miaka ya nyuma timu ya hapa Mwanza ya Alliance,siyo mgeni na anarudi nyumbani kwa mara nyingine kuja kuinoa Pamba Jiji FC,karibu sana na tutakupa ushirikiano wa kutosha," Mhe.Sima Constantine Sima,Meya wa Jiji la Mwanza.
Timu ya Pamba Jiji FC mara ya mwisho kucheza Ligi kuu ni mwaka 1999 iliposhuka daraja.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.