RC MAKALLA AMUAGIZA MGANGA MKUU WA MKOA KUWEKA UTARATIBU WA KUSHIRIKIANA NA MADAKTARI BINGWA WA BUGANDO KWENYE HOSPITALI ZA WILAYA
*Ataka uwekwe utaratibu maalum kwa kushirikiana na Hospitali za Rufaa ili huduma za kibingwa zikatolewe wilayani*
*Amshukuru Mhe. Rais Samia kwa kutenga fedha nyingi kwenye miradi ya Maendeleo*
*Aagiza kupimwa kwa maeneo ya Taasisi za Umma ili kuepusha migogoro ya Ardhi*
*Awataka viongozi kusimamia ukamilishaji wa miradi kwa wakati uliopangwa*
*Awaagiza viongozi kutoka Ofisini kukagua miradi kwa kina*
*Awataka wazazi kupeleka watoto shule ili wakapate elimu*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe CPA Amos Makalla amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa kupitia kwa Mganga Mkuu kuweka utaratibu wa kushirikiana na Madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando na Rufaa Mkoa Sekou Toure ili waweze kutoa huduma bobezi kwenye hospitali za Wilaya.
CPA Makalla ametoa agizo hilo mapema leo Oktoba 13, 2023 alipokua akikagua mradi wa Jengo la kuhifadhia Maiti lililojengwa kwa zaidi ya Milioni 149 Kati ya Shilingi Milioni 500 zilizotolewa na Serikali kuu kwa ajili ya uboreshaji wa Miundombinu kwenye hospitali ya wilaya ya Nyamagana.
Makalla amebainisha kuwa Mkoa wa Mwanza unashika nafasi ya pili kwa uwingi wa watu na Maendeleo nchini na kwamba wananchi wa wilaya za pembezoni wana uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa hivyo ni wakati sasa wa kuwatumia wataalamu kutoka kwenye hospitali za kibingwa zilizopo Nyamagana kufika wilayani na kuhudumia wananchi.
"Mganga Mkuu wa Mkoa nakuagiza, weka utaratibu wa kuwawezesha madaktari wetu kutoka kwenye hospitali za Rufaa kanda na Mkoa ili wafike kwenye wilaya zetu wakatoe huduma za kibingwa huko maana wananchi wengi wanasafiri kuja hapa mjini sasa tuone namna ya kuwafuata huko." CPA Makalla.
Akitoa taarifa ya uboreshaji wa Miundombinu kwenye hospitali hiyo Mganga Mkuu wa Wilaya Sebastian Pima amefafanua kuwa fedha zilizobaki zinatarajiwa kujenga kwa awamu jengo la ghorofa tano litakalokuwa na huduma za Mionzi, uzazi, maabara na dharula na kwamba litagharimu Bilioni Saba na kwamba kwa mwaka unaoendelea zimetengwa Milioni 800.
Awali akikagua ujenzi wa Madarasa kwa mfumo wa ghorofa kwenye shule ya Sekondari Mkuyuni Mhe. Makalla amewapongeza Jiji la Mwanza kwa utekelezaji wa mradi huo hasa kwa njia ya ghorofa ambayo imeokoa rasilimali fedha na ardhi kutokana na kubeba madarasa mengi kwenye eneo moja.
"Namshukuru sana Mhe. Rais kwa kutuletea fedha maana naambiwa mnajenga zaidi ya madarasa 400 kwa wakati mmoja, niwapongeze pia Nyamagana kwa kujenga madarasa haya kwa mfumo wa ghorofa, angalieni madarasa haya mengine yalivyochukua eneo kubwa lakini hapa kwenye eneo dogo tu yanajengwa madarasa mengi, na nimefurahishwa na taarifa ya kwamba mnajenga kwa mfumo huu kwenye shule 13." CPA Makalla.
Vilevile, Mhe Mkuu wa Mkoa ameiagiza halmashauri hiyo kupima maeneo ya taasisi za umma kama hospitali, ofisi za kata na mitaa, shule, majosho, masoko na machinjio kuhakikisha zinapata Hati ili kuepusha migogoro ya ardhi inayotokana na wananchi kumega maeneo ya ardhi.
Halikadhalika, amewataka wanaohusika na ujenzi kuhakikisha wanatekeleza miradi kwa wakati uliopangwa na viongozi kuhakikisha wanatoka ofisini na kutembelea miradi ili kuhakikisha na shughuli zinazoendelea wanazifahamu kwa kina ili kuepuka athari za kubomoa katika kurekebisha Miundombinu na samani kwenye miradi.
Akikagua ujenzi wa shule mpya ya Ng'wang'hwalanga iliyo kwenye kata ya Buhongwa B kwa zaidi ya Milioni 540 Mhe. Makalla amewapongeza wilaya na uongozi wa shule hiyo kwa usimamizi mzuri uliofanikisha ujenzi wa vyumba 14 vya Madarasa ya Msingi, 2 vya awali, matundu 14 ya vyoo vya msingi, 6 vya awali, 3 vya utawala, samani, kichoma taka na madawati 420.
"Kwa Miundombinu mizuri hivi, sio kwamba nimekagua tu bali nimekabidhiwa Ili shule yetu hii nzuri ya BOOST itunzwe vizuri na watoto wetu wapate elimu bora, naagiza ujengwe uzio na TARURA nataka muweke mipango mizuri ya kuboresha barabara ya kuingia na kutoka kwenye shule hii" amesisitiza Mkuu wa Mkoa wakati akizungumza na wananchi wa Buhongwa B.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.