RC MAKALLA ARIDHISHWA NA MANDHARI YA SOKO KUU LA MJINI KATI LINALOENDELEA KUJENGWA.
*Amuhimiza Mkandarasi kulikamilisha kwa wakati.
*Autaka uongozi wa Jiji kupunguza minada ili mzunguko wa kibiashara uwe mzuri kwa wafanyabiashara wa soko kuu.
*Asisitiza pia kwa wenye ulemavu kupewa kipaumbele wa vizimba soko kuu
Mkandarasi Mohammed Buiders anayejenga Soko Kuu la mjini kati ametakiwa kufanya kazi kwa kasi zaidi kwa lengo la wafanyabiashara waanze kufanya shughuli zao kwenye mazingira ya kisasa zaidi.
Akizungumza leo na uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza pamoja na Mkandarasi wa soko hilo mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Mhe.CPA Amos Makalla amesema ameridhika na mandhari ya soko hilo jambo la msingi sasa ni wananchi kuharakishiwa huduma.
"Hili ni soko la mfano linalokwenda na hadhi ya Jiji letu la Mwanza,nimejionea maeneo yote ni ya kisasa na ukubwa wa huduma za aina mbalimbali",CPA Makalla.
Amesema amesikia taarifa ya ujenzi huo utakamilika Septemba mwaka huu baada ya kuomba kuongezewe muda,na ana matumaini kazi hiyo itakamilika kwa wakati na ataendelea kufuatilia.
Aidha ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji kuona namna ya kupunguza minada inayofanyika maeneo mengi Jijini humo ili kuwepo na mzunguko mzuri wa kibiashara kwa wafanyabiashara kwenye soko hilo litakapoanza.
"Nilifanya mazungumzo na nduge zetu wenye ulemavu nawakumbusha uongozi wapewe kipaumbele kwa kutengewa maeneo yao kwenye soko hili kusiwepo na aina yoyote ya ubaguzi",amesisitiza Mkuu huyo wa Mkoa
Awali akimkaribisha Mkuu huyo wa Mkoa,Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana,Mhe.Amina Makilagi amesema mara baada ya kukamilika kwa soko hilo litapunguza bugudha wanayopata wafanyabiashara ndogo ndogo ambao bado wapo wengi mitaani.
"Soko hilo litachukua jumla ya wafanya biashara 1,400 watapata nafasi kwenye maduka 472 ya wafanyabiashara wadogo,wa kati na wakubwa",Mhe. Amina Makilagi,Mkuu wa Wilaya Nyamagana.
Kwa upande wake Mbunge wa Nyamagana Mhe.Stanslaus Mabula amebainisha wanamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuuwezesha Mkoa wa Mwanza miradi mbalimbali ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Zaidi ya Shs Bilioni 23 zimegharimu ujenzi wa soko hilo ambalo hadi sasa limefikia asilimia 90.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.