RC MAKALLA ASHAURI TANROADS KUMUONDOA MKANDARASI WA BARABARA YA SENGEREMA- NYEHUNGE
*Amtaka TANROADS kumuondoa Mkandarasi anayejenga barabara hiyo na kumpata mwingine mara moja*
*Amempongeza Rais Samia kutoa fedha nyingi kwenye ujenzi wa Miundombinu mkoani humo*
*Amempongeza Mwenyekiti wa CCM kwa ushindi na amemuahidi ushirikiano wa Serikali*
*Awataka MaDC, MaDED,TANROADS na TARURA kudhibiti taka kwenye mitaro*
*Amewaelekeza Kamati za Usalama za Wilaya kwa kushirikiana na Kamati za Maafa kuwa tayari na majanga*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) kumuondoa mkandarasi AVM Dillingham aliyepewa kazi ya ujenzi wa barabara ya lami ya Sengerema - Nyehunge (54.4KM) kwa zaidi ya Bilioni 73 kutokana na kuchelewa kuanza ujenzi huo tangia Mwezi Agosti na apatikane mkandarasi mweingine anapatikana na kuanza kazi mara moja.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa agizo hilo mapema leo tarehe 07, 2023 wakati wa Kikao cha kwanza cha Bodi ya Barabara Mkoa kwa Mwaka wa 2023/24 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mahususi kwa ajili ya kujadili maendeleo ya sekta hiyo.
"Mhe. Rais ametuletea fedha nyingi sana kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara ambayo nimeiona mwenyewe kwa macho nilipokua kwenye ziara ya kusikiliza kero, Mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya Nyehunge- Sengerema kwa Bilioni 70 ameshapatikana lakini hajaanza kazi sasa naagiza TĂ€NROADS kumuondoa mara moja." Mkuu wa Mkoa.
Ameongeza pia miradi ya ujenzi wa barabara za Kayenze- Airport na Kwimba Magu ambazo zinaanza kujengwa kwa Kilomita 10 na Ngudu- Mabuki kwa Kilomita 3 pamoja na Bilioni 32 zilizotolewa kujenga vivuko vipya na kukarabati vya zamani sambamba na Bilioni 30 zilizotolewa za ujenzi wa Jengo la abiria katika kuufanya uwanja huo kuwa wa Kimataifa.
Vilevile, Mhe. Mkuu wa Mkoa Awataka TANROADS na TARURA kufanya usafi kwenye mitaro ili kuondoa takataka zinazozuia maji kutoririka vema kwenda ziwani ili kuweka hali ya usalama kwa kaya zisivamiwe na maji yanayotuama sehemu mbalimbali.
Kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, CPA Makalla amezitaka kamati za usalama za Wilaya kwa kushirikiana na kamati za maafa kuwa tayari kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea hususani Elnino kwani tayari mikakati ilishawekwa kwa usimamizi wake.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amempongeza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza kwa ushindi wa kishindo alioupata kwenye Uchaguzi wa Chama hicho uliofanyika juma lililopita kufuatia kuhamishwa kwa mwenyekiti wa awali kwenda Masasi Mkoani Mtwara kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri.
Mhe. Michael Masanja, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza ametumia wasaa huo kuwashukuru wanachama wa chama hicho kwa kumchagua kwa kishindo kuwa Mwenyekiti kwenye uchaguzi na amewataka wadau wa sekta hiyo kuendelea kusimamia vema barabara na kulipa fidia kwa wakati kwenye miradi ya ujenzi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.