RC MAKALLA ATOA MAAGIZO KUKITHIRI KWA MIGOGORO YA ARDHI JIJI LA MWANZA
*Awataka watumishi wa Idara ya Ardhi kubadilika na kushughulikia kero za wananchi mapema*
*Ameliagiza Jiji la Mwanza kuhakiki na kulipa fidia kwa maeneo yaliyotwaliwa na Serikali*
*Aagiza Halmashauri ya Jiji kuzingatia mpango kabambe wa Ujenzi*
*Ayataka makampuni ya Ulinzi kuzingatia sheria na kanuni kwa wanaowaajiri*
*Awaagiza watendaji wa Serikali kuwa wepesi kusikiliza wananchi wakati wote na kuwasaidia*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ameanza ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kukagua miradi ya Maendeleo kwenye halmashauri zote za mkoa huo ambapo leo Oktoba 12, 2023 amewasikiliza wananchi wa Nyamagana kwa zaidi ya saa nane (8).
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Makalla amewataka watumishi wa Idara ya Ardhi-Jiji la Mwanza kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake watatue changamoto za wananchi ili kuepusha migogoro.
Amesema, kukithiri kwa kero za ardhi katika mkutano wake ni ishara kwamba idara hiyo haifanyi kazi zake ipasavyo na kwamba jambo hilo limepelekea jamii kukosa Imani nao kwani kumekua na urasimu usio na lazima ambao umekua ukikwamisha kusonga mbele kwa sekta hiyo.
"Jiji la Mwanza lina migogoro mingi ambayo imechangiwa na watendaji wa idara hiyo kutotatua kero za wananchi na badala yake kunakua na urasimu kwenye kushughulikia, napenda niwaambie kwamba kwa sasa mambo hayo hayana nafasi nataka muende na falsafa ya kushughulikia kero." CPA Makalla.
Vilevile, Mhe. Makalla ameagiza kuhakikiwa kwa maeneo yaliyotwawaliwa na Serikali kama maeneo ya shule pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya ili yalipwe fidia na kuwe na mpango wa kuhakiki na kulipa mara moja na sio kulimbikiza usuluhishi hadi kupelekea migogoro.
Aidha, amewaagiza jiji hilo kuzingatia mpango kabambe wa Ujenzi ili kuepusha athari za ujenzi holela na uchafuzi wa mji kwa kuruhusu mabadiriko yasiyostahili ambayo hupelekea ujenzi holela na kuharibu mandhari ya jiji hilo.
CPA Makalla ametumia pia wasaa huo kuwataka wamiliki wa makampuni ya ulinzi mkoani humo kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi ili kuwa na ajira zinazozingatia sheria na kuepusha migogoro.
"Msiogope hii ni fursa yenu ya kuonana moja kwa moja na Mkuu wenu wa Mkoa, njoo eleza kero yako maana nimekuja kusikiliza na kutatua kero zenu na kuwashauri pia namna ya kuepuka migogoro, nafasi hiyo ipo njooni." CPA Makalla akiwakaribisha wananchi.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amemshukuru kwa kusikiliza wananchi wa wilaya hiyo na kutatua kero zao ikiwa ni wilaya ya kwanza ya usikilizaji wa kero na akamuahidi kuwa wataendelea kusikiliza wananchi na kuwaondolea adha.
Ziara ya usikilizaji kero za wananchi imekuja kufuatia uzinduzi rasmi wa ngazi ya Mkoa uliofanywa tarehe 18 Septemba, 2023 ambapo alisikiliza kero 78 na Mhe. Mkuu wa Mkoa akaahidi kufanya ziara kabambe ya kusikiliza wananchi kwenye wilaya zote ili kuwatatulia kero zao.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.