RC MAKALLA ATOA MAAGIZO KWA JESHI LA POLISI MKOANI MWANZA
*Aagiza utoaji wa taarifa sahihi za uhalifu na wahalifu*
*Kutambua wageni wanaoingia na kutoka katika mitaa na kuwasajili*
*Atoa wito kwa Jamii kuacha vitendo vya kutembea na fedha nyingi*
*Ataka Ulinzi wa watoto uimarishwe kwenye jamii na kupinga natendo ya ukatili*
Leo Agosti 02, 2023 Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amefungua Kikao Kazi cha Uelimishaji kwa Wakaguzi Kata, Watendaji na Wadau wengine kuhusu masuala ya Ulinzi na usalama chini ya Kamisheni ya Polisi Jamii nchini.
Akizungumza kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Mhe. Makalla amelitaka Jeshi hilo kushirikiana na viongozi wengine kama Mabalozi na Watendaji wa vijiji kutambua wageni wanaoingia na kutoka katika mitaa na kuwasajili ili kupunguza uhalifu.
Akisisitiza suala hilo Mhe. Makalla ametoa rai kwa Jeshi hilo kuhakikisha wanaendelea kuunganisha jamii na jeshi hilo katika kuhakikisha kila mmoja nchini anakua sehemu ya polisi jamii kwani wananchi ni muhimu sana kwenye masuala ya usalama.
Vilevile, amekemea tabia ya baadhi ya wananchi ya kutembea na fedha nyingi wakiona ni sifa, na badala yake amewataka kuweka fedha hizo Benki kwani wahalifu wanapata matamanio ya kufanya uhalifu wanapokua na taarifa za mtu fulani kutembea na fedha nyingi.
CPA Makalla ameagiza ushirikiano baina ya jeshi hilo na vyombo vingine ili kuhakikisha uhalifu unaondoka nchini na ametoa wito kwa Wakaguzi Kata kufanya kazi kwa weledi pasipo kuonea mtu kwa kushirikiana na viongozi wengine ili kuhimarisha usalama.
"Nafurahia kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, nakushukuru sana Kamishna wa Polisi Jamii kwa kuongoza kwa vitendo maana Maafisa Watendaji wa Kata kuwapo hapa leo ni ishara ya kufanya kazi kwa vitendo." Amesisitiza Mhe. Makalla baada ya kujinasibu kukomesha wizi wa vifaa kwenye mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR).
Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kutoa taarifa za uongo za hali ya uhalifu na wahalifu na kuacha kufanya ramli chonganishi kwenye jamii pamoja na kuwalinda watoto na jamii kwa ujumla dhidi ya matendo ya Ukatili.
Naye Mkuu wa Kamisheni ya Polisi Jamii nchini, Kamishna Faustine Shilogile ametoa rai kwa watendaji kutoa ushirikino kwa Jeshi hilo ili kufanikisha lengo la dhana ya kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo na amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuimarisha zaidi ulinzi kwenye maeneo yote.
Kikao Kazi hicho cha siku tatu kilichowakutanisha pia na wadau wengine kama mashirika yasiyo ya Kiserikali kinaongozwa na kauli mbiu isemayo 'Polisi Jamii kwa Usalama na Maendeleo yetu'.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.