RC MAKALLA ATOA MAAGIZO KWA WATAALAM WA KILIMO KUONGEZA TIJA ZAO LA PAMBA NA UTOSHELEVU WA CHAKULA MWANZA
*Ataka mkakati wa kuhakikisha Tija inaongezeka kwenye Mazao hususani Pamba*
*Aagiza Maafisa Ugani kutimiza Majukumu yao ya Msingi ya kuelimisha wakulima*
*Awaagiza Wakurugenzi kuwawezesha Maafisa Ugani nao kuwajibika kuwafikia wakulima*
*Awataka Mawakala kusogeza maduka ya Mbolea kwa Wakulima*
*Aagiza wataalam wa kilimo kujengewa uwezo ili kupeana uelewa*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wataalam wa Kilimo kuhakikisha wanaweka
Mikakati ya kuongeza Tija kwenye uzalishaji wa zao la Pamba na Mazao ya Chakula ili Mkoa uwe na utoshelevu wa chakula na kuinua uchumi.
CPA Makalla ametoa wito huo mapema leo Disemba 20, 2023 kwenye Mkutano wake na Wadau wa Kilimo ikiwa ni muendelezo wa Vikao kazi vya kisekta vya kujadili namna ya kuongeza tija ambapo kupitia Kikao hicho ameagiza Uzalishaji wa Kisasa wa Mazao ya Chakula na biashara hususani pamba.
Mkuu huyo wa Mkoa ameongeza kuwa mradi wa vijana kwenye kilimo kupitia programu ya Kesho Bora Zaidi unaoratibiwa na Wzara ya Kilimo ni lazima uenziwe kwa kujitambulisha kuwa zao lipi ni la biashara na linategemewa kuwainua kwenye uchumi wananchi wengi na zao gani ni la pili kwa uzalishaji Mwanza.
"Mwanza hatupaswi kwenda shaghalabagala ni lazima tutimize wajibu wetu ili ufike wakati tujitambulishe kwa kuwa na zao letu kuu la biashara, hivyo Maafisa ugani na wataalam kutoka Mkoani ni lazima tuwe na Mkakati wa kuinua kilimo kwa wananchi wetu." Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Amesema zao la pamba limekua likishuka kwa uzalishaji mwaka hadi mwaka pamoja na kuwa na ardhi ya kutosha na mifugo haifanyi vizuri hilo ni jambo baya kwa maendeleo ya Taifa na kwamba tumefika hapo kutokana na wataalam katika kata kutokua na mkakati wa kusaidia wakulima kwa kuwafundisha kanuni bora za kilimo pamoja na mazao mengine ya chakula.
"Tunataka Ekari Moja ya shamba izalishe kilo elfu 1 ya Pamba na sio kilo 200 wanazopata wakulima hivi sasa kwani hata Mhe. Rais katika kuhakikisha zao hili linaimarika amehakikisha wataalam wa kilimo wana usafiri wa kuwafikisha moja kwa moja shambani, sasa Wakurugenzi ni lazima muwajibike kwa kuwapatia mafuta." Mhe. Makalla.
Aidha, Makalla amesema taasisi kama TOSC, Taasisi ya Utafiti TARI Ukiriguru, Taasisi inayosimia Ubora wa Udongo, Chuo cha Kilimo cha Ukiriguru na Shamba la Mifugo Mabuki ambazo zipo Mwanza ni lazima ziwajibike ilivyokusudiwa na kuonesha uwepo wake wa kuwasaidia wakulima kuongeza tija kwenye mazao.
"Udongo na Mbegu bora zinaweza kutupa matokeo mazuri sana kwenye kilimo na katika hilo Mhe. Rais ameonesha kwa mfano kwenye ruzuku na kuimarisha taasisi mahsusi inayoshughulikia Mbegu ili kuwe na uzalishaji mzuri wa mazao na uwepo wa Maduka ya mbolea jirani na wakulima." Mkuu wa Mkoa.
Afisa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkoa Innocent Keya amebainisha kuwa Mahitaji ya Usambazaji wa Pembejeo za Pamba 2023/24 Mkoa umekadiria kutumia tani 1.972 za mbegu za Pamba na Chupa 901,036 za viuadudu na kwamba hadi kufikia Disemba 04, 2023 tani 1.742 za Mbegu zimesambazwa Halmashauri zinazolima Pamba na tani 1, 671 zimegawiwa kwa wakulima.
"Kufikia Juni 2023 wakulima 36, 992 wamesajiriwa katika Mfumo na hadi kufikia Disemba 18, 2023 wakulima 58, 596 walikua wamesajiriwa na 4, 362 walikua wamenunua mifuko 37, 282 (Tani 1.864) ya Mbolea." Amesema Keya wakati akizungumzia Changamoto za Kilimo Mwanza ikiwemo upungufu wa Maafisa Ugani kwa 260 kati ya 755 wanaohitajika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.