RC MAKALLA ATOA MAAGIZO KWA WAVAMIZI WA SHAMBA LA MIFUGO MABUKI-MISUNGWI
*Aagiza uongozi Mabuki, jeshi la polisi wilayani humo kufanya ukaguzi kubaini wavamizi wote*
*Asema Rais Samia anaziishi fikra za Mwl Nyerere kwa kutoa Ng'ombe jike (Mitamba) 500*
*Awapongeza wanafunzi wa BBT kwa mafunzo mazuri ya ufugaji wa kisasa*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amelitaka jeshi la polisi wilayani Misungwi kwa kushirikiana na uongozi wa shamba la mifugo la Mabuki kuweka mipaka ya eneo lote la hekari elfu 25 na kuwabaini wavamizi ili mkuu wa wilaya hiyo awaondoe mara moja kwa ustawi wa shamba hilo.
Ametoa agizo hilo leo tarehe 18 Januari, 2024 wilayani Misungwi baada ya kupokea changamoto ya wananchi wakiwa na mifugo mingi kuvamia shamba hilo na kuathiri shughuli za utafiti, uzalishaji na Utoaji wa mafunzo kwa wafugaji jambo linalofanywa na wananchi kutoka kwenye kata nne zinazozunguka shamba hilo.
"Malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hii na kuenzi fedha nyingi anazozileta Mhe. Rais Samia kwenye shamba hilo lazima ziwe na tija maana wavamizi ndio wanaotaka taasisi hii ife, vijana wa mradi wa BBT LIFE wasifanikiwe, mifugo yetu ife kwa magonjwa na hatutakubali kufika huko." CPA Makalla.
Aidha, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ng'ombe majike 500 (Mitamba) kwenye shamba hilo ambao wamesaidia kuendeleza uzalishaji na kutolea mafunzo kwa wafugaji ya namna bora ya kuzalisha nyama na maziwa bora kupitia mafunzo ya muda mfupi na mrefu yatolewayo shambani hapo.
Aidha, awapongeza wanafunzi walio kwenye shamba hilo chini ya mradi wa Jenga Kesho Bora (BBT) kwa mafunzo mazuri waliyoyapata na akabainisha kuwa uvumilivu wao utawasaidia kujiajiri kwa kufanya shughuli za uzalishaji kupitia ufugaji wa kisasa waliojifunza.
Mhe. Paul Chacha, mkuu wa wilaya ya Misungwi ametoa onyo kwa wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye shamba hilo kuacha mara moja ili kuhakikisha utafiti, uzalishaji na mafunzo yanafanikiwa kwa mujibu wa sheria za uanzishwaji wa shmaba hilo la mifugo.
Meneja wa Shamba hilo Leni Mwala ametumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia kwa kuendeleza shamba hilo lililoanzishwa mwaka 1967 lenye hekari elfu 25 kwa kuwaletea ng'ombe jike 500 (Mitamba) mwaka 2022/23 ambao wamesaidia kuendeleza wafugaji na kujifunzia.
"Serikali ya awamu ya Sita imetushangaza kwa furaha maana inatimiza maono ya Baba wa Taifa letu Hayati Rais Nyerere kwa kutuletea Mitamba 500 jike kwa ajili ya kuwakuza na kutumika kuendeleza kwenye utafiti kwa manufaa ya jamii ya wana Mwanza." Mwala.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.