RC MAKALLA ATOA ONYO KWA WANANCHI WANACHUKUA SHERIA MKONONI NA KUHATARISHA USALAMA
*Amewataka wananchi kufuata sheria na kutumia mahakama kuwasilisha madai yao*
*Awaagiza Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo kuweka mpango wa amani wakati wote*
*Atoa wito kwa wanaMisungwi kujiandaa na Fursa zitokanazo na Reli ya Kisasa*
*Amemshukuru Rais Samia kwa kujenga Mradi wa Maji utakaowanufaisha Misungwi*
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kuhatarisha usalama kwa jamii kutokana na tukio lililotokea mwezi Oktoba katika kijiji cha mwaniko Wilayani Misungwi la vijana wawili kuchomwa moto na kundi la wananchi wakidaiwa kuiba mpunga na kuku.
Mkuu wa mkoa Makalla ametoa rai hiyo mapema leo Novemba 6, 2023 wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wake wakati akisikiliza na kutatua kero za wananchi Wilayani Misungwi ikiwa ni ratiba yake aliyojipangia ya kuwafuata wananchi kwenye wilaya zote tangia alipozindua rasmi zoezi hilo mwezi Septemba mwaka huu.
Makalla amesema Mahakama ndicho chombo cha kisheria kinachotoa haki hivyo wananchi wanapokua na jambo wanapaswa kulifikisha mahakamani ili likasikilizwe na kupatiwa maamuizi ya kisheria na amefafanua kwamba zaidi ya wananchi 35 wamekamatwa kutokana na kujihusisha na tukio hilo ovu kwa watu wasio na hatia.
"Nitoe Onyo kwa wananchi kutochukua sheria mkononi, chombo kinachotoa haki ni mahakama hivyo nataka jambo hili lisijirudie tena na mabalozi, wenyeviti wa vijiji, watendaji wa vijiji na kata pamoja na viongozi wote tushirikiane kulinda amani" Makalla.
Aidha, amewaagiza Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo kuketi na viongozi wa ngazi zote kuanzia kwenye vitongoji kuwekeana mikakati ya kuhakikisha kunakua na amani wakati wote ndani ya vijiji, kata, tarafa na wilaya kwa ujumla.
Vilevile, Mhe. Makalla amewataka
wananchi wa Misungwi kuchangamkia fursa zinazoletwa na Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwani kwenye kituo cha Fella patakua ndipo kituo cha kupakia na kushusha mizigo kabla ya kusafirishwa kwenda kwenye mikoa na nchi za jirani.
Halikadhalika, Mhe. Makalaa ametumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia kwa kujenga mradi mkubwa wa maji wa Butimba unaotarajia kuwapatia maji wananchi wa Misungwi na ujenzi wa barabara fupi ya kwenda Kahama unaotarajiwa kuanza siku za usoni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.