RC MAKALLA ATOA SIKU 42 KWA MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI WA AWAMU YA KWANZA YA JENGO LA HALMASHAURI KWIMBA
*Asema Mkandarasi huyo hataongezewa tena muda wa ujenzi wa jengo hilo*
*Awaagiza Halmashauri hiyo kuondoa changamoto kwenye ujenzi huo kwa kufanya malipo kwa wakati*
*Amshukuru Rais Samia kwa kuidhinisha zaidi ya Bilioni 4 kujenga Makao Makuu hayo*
*Awapongeza Kwimba kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, awaahidi Madaktari bingwa kutoa huduma hapo*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Makalla amemtaka Mkandarasi Kwiyera Interprises Limited kukamilisha ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kufikia Disemba 31, 2023 ili awamu zingine za ujenzi ziendelee na kuwapatia watumishi na wananchi huduma nzuri.
Ametoa agizo hilo mapema leo akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo kwenye wilaya hiyo alipotembelea ujenzi huo unaofanyika kwenye kata ya Ngudu kwa zaidi ya Bilioni 4 ambapo bilioni 1.3 zitatumika kwa awamu ya kwanza.
"Mkandarasi leo umechelewa na umeshaongezewa mara nne muda wa kukamilisha nami kwa kuzingatia ucheleweshaji wa malipo ya fedha kwa mkandarasi huyo nakutaka sasa ukamilishe jengo ili hadi Disemba 30 mwaka huu." Mhe. Makalla
Aidha, Makalla amemshukuru Rais Samia kwa kutenga fedha zaidi ya Bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo (Bilioni 1.3 awamu ya kwanza) ambalo amebainisha kuwa litasaidia kuwaweka watumishi kwenye mazingira nadhifu ya kufanyia kazi na wananchi kupata huduma safi.
Vilevile, amewaagiza idara ya ujenzi na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kusimamia ili mkandarasi awepo eneo la kazi wakati wote na kwamba asipo kamilisha hadi kufikia wakati huo atapewa adhabu kwa sheria na akamuahidi mkandarasi huyo kuwa ifikapo Januari 03, 2024 atafika kukagua.
Awali Mkuu wa Wilaya ya kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija alifafanua kuwa Mkandarasi huyo amekua na mwenendo wa kusuasua kwenye ujenzi hadi kufikia hatua ya kuongezewa muda kwa mara tatu baada ya muda wa awali kuisha kwa mujibu wa mkataba pamoja na kupatiwa fedha.
Akikagua hali ya utoaji huduma kwenye Hospitali ya Wilaya inayojengwa kwa zaidi ya Bilioni 3.8 kwenye eneo la Icheja kuanzia mwaka 2018/19 CPA Makalla amewapongeza Kwimba kwa kukamilisha ujenzi ambapo wagonjwa zaidi ya 475 wanalazwa kwa mwezi na kusaidia mtiririko wa huduma.
"Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha za ujenzi na vifaa vya kisasa, tunatambua kazi nzuri inayofanywa na wataalamu wa afya ila lazima tusimamie matumizi ya lugha nzuri kwa wagonjwa kwani inaleta matumaini hata kabla ya kuanza kutoa huduma yenyewe" Amesisitiza CPA Makalla.
Akitoa taarifa ya ujenzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Happness Msanga amebainisha kuwa fedha hizo zilitoka kwa ajili ya ukarabati wa iliyokua hospitali ya wilaya eneo la kakora lakini kutokana na ufinyu wa eneo waliamua kujenga hospitali mpya kwenye kata ya Ngudu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.