RC MAKALLA AWAOMBA VIONGOZI WA DINI NA MILA KUELIMISHA JAMII KUEPUKA RAMLI CHONGANISHI
*Chanzo cha matukio ya mauaji yanasababishwa na ramli chonganishi Na imani Za kishirikina*
*Aagiza Watumishi kudumisha nidhamu mahala pa kazi*
*Atoa ratiba ya kusikiliza kero za wananchi kila wilaya*
*Amemshukuru Mhe. Rais kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya Maendeleo*
*Asisitiza ukusanyaji Mapato na matumizi kwa mujibu wa sheria*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makalla ametoa rai kwa viongozi wa wilaya ya Magu kushirikiana naye katika kuwahudumia wananchi katika majukukumu ya kila siku.
Mhe. Makalla ametoa wito huo leo Juni Mosi, 2023 mbele ya viongozi, watendaji na makundi mbalimbali wilayani humo alipofika kwa ziara ya kikazi ya kujitambulisha.
"Hongereni Magu mmepata maendelo makubwa ukilinganisha na kipindi cha nyuma nilipofika hapa, napiga hodi Magu na nawaomba ushirikiano maana tuna majukumu mengi ya kufanya katika kuiinua zaidi Wilaya yetu." CPA Makalla.
Aidha, amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha kunakuwa na amani wakati wote huku akibainisha kuwa kuna viashiria vya uvunjifu wa amani kutokana na kuwa na historia ya matukio yanayosababishwa na ramli chonganishi.
"Imani za kishirikina kwa mfano kuamini unaweza kupata utajiri, mifugo au mazao mengi sana huku ukiwasikiliza waganga kuwa lete kiungo fulani hiyo si sawa na machifu mtusaidie kutoa Elimu kwamba hakuna njia ya mkato ya kuoata utajiri." Makalla.
Katika kusisitiza hilo, Mhe. Makala amewaagiza viongozi na watendaji wa ngazi za chini hususani kwenye vitongoji kuwa na ajenda ya kukemea masuala ya ushirikina kwenye vikao vyao vya kila wakati.
"Kila serikali ya kijiji muweke ajenda ya kutoa Elimu ya kuachana na imani za kishirikina na ramli chonganishi, tunataka wananchi wetu wawe salama na Polisi Jamii fanyeni kazi hiyo", Amesisitiza Mhe. Makalla.
Ameongeza kuwa pamoja na mafanikio makubwa waliyopata wana wajibu wa kufanya kazi kwa uadilifu hususani kukusanya mapato na kutumia kwa mujibu wa sheria ili kuepuka hoja za ukaguzi na kutoa tumaini kwa wananchi huku wakijibu kero zao.
"Nendeni mkajipange nitakuja kusikiliza kero za wananchi, anzeni kuweka mambo sawa hususani idara ya Ardhi, Maji, mifugo mimi sio mtu wa kukaa ofisini nitakuja kusikiliza kero za wananchi mbele yenu hapa na kitakua kipimo cha uwajibikaji wenu kama kweli mnawahudumia vizuri." CPA Makalla.
Vilevile, Mhe. Mkuu wa Mkoa ametumia wasaa huo kutoa pongezi na shukrani kwa Mhe. Rais kwa kupeleka fedha nyingi wikayani humo kwa ajili ya kutekeleza miradi ya Maendeleo katika kila Sekta.
Katika wakati mwingine, Mhe. Makalla amekagua maendeleo ya Ujenzi wa jengo jipya la Kisasa la Makao Makuu ya Halmashauri hiyo na amewapongeza kwa usimamizi mzuri wa jengo hilo linalojumuisha Ofisi 72 pamoja na kumbi za Mikutano huki likigharimu Bilioni 5.7.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.