RC MAKALLA AWAPANDISHA MZUKA PAMBA JIJI FC
*Awamwagia noti wachezaji na benchi la ufundi kuelekea michezo miwili ya nyumbani*
*Awatia Shime mchezo dhidi ya TMA kutoka na ushindi nyumbani*
*Asema Pamba FC inastahili kukaa kwenye nafasi za juu katika msimamo wa Ligi ya Championship*
*Abainisha kuwaleta wachezaji wanne kwa Majaribio kutoka Congo DRC kwenye Dirisha dogo la usajili*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla leo Disemba 7,2023 ameitembelea kambi ya timu ya soka ya Pamba Jiji FC inayoshiriki Ligi ya Championship na kuwapa motisha ya Shilingi Milioni 4, ambapo 3 kwa wachezaji na 1 kwa benchi la ufundi kutokana na kuwa na matokeo mazuri katika michezo yao ya hivi karibuni.
Akizungumza na wachezaji hao iliyopo kambini hapo kwenye Mtaa wa Iseni nje kidogo ya Jiji la Mwanza, Mkuu huyo wa Mkoa amewapongeza wachezaji hao kwa kupambana vizuri dimbani na kushika nafasi ya tatu ikiwa na mtaji wa pointi 27.
"Kwa hadhi ya Pamba Jiji nafasi tuliyonayo ya pili nikiwa na maana Jumapili hii tunashinda na kushika nafasi hiyo ndiyo tunastahili na tusishuke bali tupande juu, "amefafanua Mkuu huyo wa Mkoa ambaye ni mlezi wa timu hiyo.
Ameongeza kuwa wakati wa dirisha dogo atawaleta wachezaji wanne kutoka Congo DRC na kama dawati la ufundi litaridhika nao watasajiliwa kwa lengo la kuiongezea nguvu Pamba Jiji FC.
"Mhe Mkuu wa Mkoa tunaendelea kukuahidi kufanya vizuri katika michezo yetu na kutimiza lengo letu la kupanda Ligi kuu msimu ujao,tunakushukuru kwa kushikamana nasi,"Alhaji Majogolo,Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji FC.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA ndugu Peter Leti amesema kambi ya timu hiyo inaendelea vizuri na maelekezo yote anayotoa wanayazingatia hali ambayo yameleta matokeo chanya hadi sasa.
Nahodha wa wana TP Lindanda Jerryson Tegete akipokea kitita cha Shs milioni 3 kwa niaba ya wachezaji wanzake kutoka kwa mkuu wa Mkoa,amesema watazidisha ari ya kufanya vizuri ili kutimiza nia yao ya kucheza Ligi kuu.
"Mhe Mkuu wa Mkoa mchezo wetu dhidi ya TMA nakuahidi tutafanya vizuri kwani kasoro ndogo za kiufundi upande wa umaliziaji nimeufanyia kazi," Mbwana Makatta kocha mkuu wa Pamba Jiji FC.
Timu ya Pamba Jiji FC itashuka dimbani Nyamagana Jumapili hii kumenyana na TMA inayotokea Arusha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.