RC MAKALLA AWAPONGEZA TRA NA WALIPA KODI MKOA WA MWANZA KUVUKA LENGO LA MAKUSANYO YA KODI 2022/23
*Wakusanya zaidi ya Bilioni 269 na kuvuka lengo la Makusanyo kwa Bilioni 48 zaidi*
*Atoa wito kwa wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi*
*Ayataka mashirika na taasisi za umma kuwa mfano wa kuigwa kwa kulipa kodi kwa wakati*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wafanyabiashara kulipa kodi sahihi kwa mujibu wa sheria na kwa hiyari ili Serikali iendelee kuwahudumia wananchi kupitia utoaji wa huduma bora za kijamii kama Maji, Elimu, Nishati ya Umeme, Barabara na Afya.
Mhe. Makalla ametoa pongezi hizo kwenye halfa ya wiki ya mlipa kodi iliyofanyika jioni ya leo tarehe 05, Disemba 2023 kwenye Ukumbi wa Gold Crest Mkoani humo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Mwanza kwa wateja wao.
"Maendeleo yoyote yanayofanywa na Serikali ni fahari kwa walipa kodi hivyo ni lazima kila mfanyabiashara awe na kiu ya kuwa mdau kwenye kuchangia maendeleo ya Taifa lake na TRA endeleeni kutoa elimu kwa walipakodi na wananchi kwa kutumia mifumo" Makalla.
Aidha, amewapongeza Mamlaka ya Mapato Mkoani humo na walipa Kodi kwa kuvuka lengo la ukusanyaji 2022/23 kwa kukusanya Bilioni 269.78 ikiwa ni Bilioni 48 zaidi ya makisio na kwamba rekodi hiyo imefanya wafikishe zaidi ya asilimia 105 ya mapato waliyokusudia kukusanya.
Aidha, ametumia hafla hiyo kuwataka viongozi wa taasisi za uma kuwa mabalozi wa kulipa kodi na kuhimiza watumishi walio chini yao kulipa kodi halali na kwa wakati kwa kutumia risiti za kielektroniki ili kuendea kuwa na Taifa imara linalojitegemea.
Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa TRA nchini Kayobyo Majogoro amesema wanajivunia mfumo dhabiti wa kodi unaowaweka karibu na wafanyabiashara na wawekezaji nchini kwa kulipa kodi bila shuruti na kuwa na mchango mkubwa kwenye kufikia lengo la Serikali la ukusanyaji mapato huku akiwasihi kuendelea kutumia risiti za IEFD kwenye biashara.
"Katika mwaka wa fedha uliopita Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Mwanza umekusanya Bilioni 269.78 ikiwa ni sawa na mafanikio ya asilimia 105, makusanyo haya ni ongezeko ya Bilioni 48 ukilinganisha na kiwango cha mwaka uliotangulia na kwakweli tunatambua na kuwashukuru sana walipakodi wetu." Mwakilishi.
"Hafla ya kuwapongeza walipakodi mkoani mwanza ilianza jana kwa kuwatembelea wagonjwa Nyamagana Hospitali na kuwaona wagonjwa pamoja na kuwapatia msaada mbalimbali na asubuhi ya leo tumefanya matembezi na michezo kabla ya kuhitimisha kwenye hafla ya usiku ya kuwapongeza walipa kodi wetu." Meneja TRA Mwanza Ernest Dundee.
Juma la walipa kodi Mkoa wa Mwanza limechagizwa na Kaulimbiu isemayo 'Kodi yetu Maendeleo yetu, Tuwajibike huku likihanikizwa na zawadi kwa wachangiaji wakubwa, wachangiaji bora na washindi wa Mkoa na Wilaya ambao wamepimwa kupitia utunzaji bora wa kumbukumbu, ushirikiano na mamlaka hiyo, matumizi sahihi ya mashine za kodi na ulipaji bora wa hiyari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.