RC MAKALLA AWATAKA USHIRIKA KUTOA ELIMU KWA WAKULIMA JUU YA FAIDA ZA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI
*Awataka vyama vya ushirika kutoa elimu ya faida za mfumo huo*
*Amesema mfumo huo unatoa uhakika wa soko la mazao*
*Aziagiza Halmashauri kukutana na wadau wilayani*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka Wadau wa ushirika kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima juu ya faida za mauzo ya mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa maendeleo ya sekta hiyo.
Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo hayo mapema leo Januari 11, 2024 wakati wa kikao cha wadau wa ushirika kilicholenga kujadili utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya choroko na dengu 2023/24.
Amesema, wakulima wanataka kuona wanapata bei nzuri kwenye mazao kufuatia kuwekeza muda na nguvu kwenye kilimo kwa msimu mzima aidha kwa mikopo kutoka kwenye mabenki hivyo wanachohitaji ni kufahamishwa manufaa ya mfumo huo.
"Serikali inatambua mchango wa mfumo huu na umesaidia kuchochea wakulima kupata soko la uhakika lenye tija, mfumo huu umesaidia wakulima kwenye mazao kama kakao, korosho na ufuta na kwamba umekuza huduma za kifedha vijijini." Mkuu wa Mkoa.
Vilevile, amefafanua kuwa Mfumo wa stakabadhi ghalani una manufaa makubwa sana na umesaidia wakulima kutumia mzani halisi na kuongeza kipato kwa misimu miwili ya 2020 hadi 2022 na sasa Serikali imejipanga kuboresha zaidi huduma ili mkulima anufaike zaidi.
Robert Sunza kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini amesema wao kama wahamasishaji na wasimamizi wa maendeleo ya ushirika na kwenye mfumo huo unasaidia kupata ubora wa bidhaa, ushindani wa bei kutoka kwa wanunuzi na kupata takwimu za uhakika.
"Vilevile mfumo wa stakabadhi za ghala unasaidia kuongeza uzalishaji, mapato, miundombinu ya uhifadhi, usimamizi pamoja na kuimarika kwa biashara kutokana na kuongezeka kwa wanunuzi." Amefafanua ndugu Sunza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.