RC MAKALLA AWATAKA WADAU MKOANI HUMO KUTOA MAONI YA KINA KWENYE DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050
*Azitaka Taasisi kuainisha Vipaumbele vya Bajeti na Maendeleo ya Jamii*
*Atoa wito kwa Sekta za Uvuvi, Kilimo cha Pamba na Uchimbaji wa Madini kushiriki kikamilifu*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka Wadau Mkoani humo kushiriki vema katika kutoa Maoni ya Kitaalamu katika kuhakikisha wanachangia vema kwenye upatikanaji wa Dira Bora ya Maendeleo 2050.
Ametoa wito huo leo tarehe 24 Julai 2023 wakati akifungua Warsha ya Uelimishaji Umma juu ya uandaaji wa Dira ya Taifa 2050 iliyowakutanisha Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala Wilaya, Wakurugenzi, Wakuu wa Seksheni na Vitengo na Wakuu wa Taasisi mbalimbali.
Makalla amesema, katika kupanga malengo ya muda mrefu kama Dira ya Maendeleo ni lazima kila taasisi iainishe Vipaumbele, Bajeti na Maendeleo ya Jamii hivyo ni lazima kuthamini fursa waliyoipata ya kuwa sehemu ya kuchangia maoni na kuitumia vema.
"Ni kikao chetu muhimu sana katika kuelekea maendeleo endelevu ya miaka ya mbele mathalani jeshi la Polisi lazima liweze kupanga linataka liwe la aina gani kwa mfano kwenye kupambana na wizi wa kimtandao." CPA Makalla.
Aidha, Mhe. Makalla amezitaka Sekta kuu za kiuchumi kama Uvuvi, Kilimo cha Pamba, Uchimbaji wa Madini kupanga vema kwenye vipaumbele mahususi vitakavyokuza sekta zao kiuchumi ili kusaidia wananchi walio wengi maana ndizo shughuli kuu za kiuchumi Mkoani humo.
"Taifa letu limekua na Dira ya Maendeleo ya kuishia 2025 na sasa Serikali ipo kwenye maandalizi ya dira kuelekea 2050 ambapo tumekutana makundi mbalimbali kwa kushirikiana na ngazi ya Taifa katika kuhakikisha kila kundi linahusika kwenye kutoa maoni." Amesema Katibu Tawala Mkoa, Balandya Elikana.
Bwana Omary Othman, Mjumbe wa Maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa amesema wanahamasisha na kutoa elimu ili kupata ufahamu wa pamoja na kwamba wanategemea viongozi wa Mkoa husika watapeleka elimu hiyo hadi chini ili wananchi waweze kushiriki vema kutoa maoni wakati wa zoezi hilo utakapofika.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.