RC MAKALLA AWATAKA WADAU WA KILIMO, UVUVI NA UFUGAJI KANDA YA ZIWA MAGHARIBI KUJIANDAA NA MAONESHO YA KISASA YA NANE NANE 2023.
*Azitaka Halmashauri zote kutoka Kanda hiyo kushiriki kwa kina*
*Atoa wito kwa Sekta za Uvuvi, Kilimo na Ufugaji kuonesha ubunifu kupitia maonesho hayo*
*Awataka Viongozi kuandaa vijana kujikita kwenye kilimo ili kujipatia uchumi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wadau wa Kilimo, Uvuvi na Ufugaji kutoka Kanda ya Ziwa Magharibi kujiandaa vema na maonesho kabambe ya Nane nane yanayotarajiwa kufanyika kwenye viwanja vya Nyamhongolo Jijini Mwanza.
Ametoa wito huo mapema leo tarehe 26 Julai 2034 wakati wa kikao cha tathmini ya maonesho ya mwaka na maandalizi ya maonesho ya kilimo (NANE NANE) na maandalizi yanayoendelea ya maonesho hayo yanayotarajiwa kufanyika Kuanzia Agosti Mosi hadi 8, 2023.
Vilevile, Makalla ametoa wito kwa wataalamu kutoka mikoa hiyo kuwasaidia wafugaji, wavuvi na wakulima katika kuongeza thamani ya mazao yao na kufanya kilimo bora kwa ujumla ili waachane na zana za zamani na uwepo wao uongeze tija kwa wakulima na kuwainua kiuchumi kwa ujumla.
"Tunapaswa katika maonesho haya wataalamu wote na wagani kuendelea kuwasaidia wavuvi ma wafugaji katika kufanya shughuli zao kibiashara ili kuinua uchumi wao, tuwafundishe wapi watapata masoko ya mazao na kuongeza thamani ya mazao." CPA Makalla.
Aidha, ametoa rai kwa viongozi na watendaji kutoka kwenye kanda hiyo kuhakikisha wanawaleta wafugaji, wakulima na wavuvi kwenye maonesho hayo ili wajifunze kwa vitendo kupitia mashamba darasa ya Uvuvi, Kilimo na Vipando vitakavyooneshwa kwenye viwanja hivyo.
Kwa mara ya tano Kanda ya Ziwa Magharibi inatarajia kuadhimisha maonesho ya Nane nane katika viwanja vya Nyamhongolo na maonesho ya mwaka 2023 yamebeba kaulimbiu isemayo "Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.