RC MAKALLA AWATAKA WANANCHI WA NANSIO UKEREWE KUTUMIA MAJI SAFI NA SALAMA
*Amshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha zaidi ya Milioni 350 kuongeza Usambazaji Maji*
*Awataka MWAUWASA kutoa Elimu kwa wananchi kutunza mradi*
*Awashauri wananchi kuachana na mazoea ya kutumia Maji ya ziwani*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wananchi wa Nansio Ukerewe kutumia maji safi na salama kutoka chanzo na kituo cha tiba ya Maji Nebuye chenye thamani ya zaidi ya Bilioni 14. 8 ili kujihakikishia afya bora na kuepukana na Magonjwa ya tumbo yatokanayo na matumizi ya Maji ya ziwani.
Mhe. Makalla amesema hayo mapema leo novemba 23, 2023 wakati wa ziara yake wilayani Nansio alipotembelea Chanzo na Kituo cha Tiba ya Maji Nebuye kilicho kwenye Usambazaji wa zaidi ya Kilomita 23.2 kwa zaidi ya Milioni 350 chini ya Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).
Makalla ametumia wasaa huo kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo ili kuboresha huduma hiyo kwa wananchi ambapo amebainisha kuwa hali ya upatikanaji wa Maji safi itaongezeka na wananchi wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo kwa kuunganisha maji kwenye nyumba zao na kuachana na matumizi ya Maji ya ziwa.
"Maji haya ndio safi na Salama kwani yametibiwa hivyo hakuna tena magonjwa ya tumbo tukiyatumia kwa hiyo nawasihi tuachane na maji ya ziwa ambayo si salama kwa matumizi na hatarishi kwa wananchi kuliwa na mamba na viboko" Makalla.
Halikadhalika, Makalla amewataka MWAUWASA kutoa elimu kwa wananchi wa Nansio ili waumiliki mradi wao na kuweza kuutunza wakijivunia kuwa Rais Samia anauboresha kwa ajili yao hivyo wanapaswa kuutunza ili uwe na tija.
Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) Mhandisi, Robert Lupoja amebainisha kuwa chanzo hicho cha maji kinahudumia wateja 3900 kwa sasa kwenye vituo vya maji 52 na kwamba wapo kwenye juhudi za kuondoa kabisa upotevu wa maji wa asilimia 10 uliopo kwa sasa.
"Wananchi wa Nansio tunaenda kuwaongezea huduma ya maji safi kupitia usambazaji huu mkubwa utakaotufikisha kwenye kuhudumia wananchi hadi kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2024/25 hivyo tunawaomba mlipe ankara za maji kwa wakati ili tuongeze usambazaji." Amesisitiza Mkurugenzi huyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.