RC MAKALLA AZINDUA KAMPENI CHANJO YA SURUA NA RUBELA, ZAIDI YA WATOTO LAKI 7 KUCHANJWA MWANZA
*Ahimiza wananchi waelimishwe athari za Surua na Rubella na ni chanjo salama*
*Ataka Sekta zote zishirikiane na hamasa iwepo kutokomeza Kipindupindu*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla leo Februari 9, 2024 amezindua kampeni ya Chanjo ya Surua na Rubella kwa watoto wa miezi 9 na chini ya miaka 4 na miezi 11 itakayoanza Februari 15-18 ambapo zaidi ya watoto laki saba watapatiwa chanjo hiyo.
Akizungumza na wajumbe wa kamati ya afya kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Makalla amehimiza elimu na hamasa ya kutosha itolewe kwa wananchi kuhusiana na athari za ugonjwa huo na chanjo hiyo inayotolewa na Serikali ni salama na haina malipo.
"Bado kuna kasumba ya baadhi ya wananchi kukimbilia tiba mbadala badala ya kwenda vituo vya afya, nawaomba sana mjitahidi kutoa elimu ya kutosha ili mpango huu uwe na tija," amehimiza CPA Makalla.
Kuhusu ugonjwa wa Kipindupindu ambao amesema hadi sasa Mkoa wa Mwanza una wagonjwa 9, huku 7 wakitokea Sengerema na 2 wapo Ilemela,ametaka kuwepo na ushirikiano na hamasa kutoka Sekta zote ili kutokomeza ugonjwa huo.
"Mkakati wa elimu kuhusiana na ugonjwa huo tuendelee kutolewa ikiwemo kunawa kwa maji yanayotiririka, kuwa na choo bora na maji salama na kuepuka mazingira machafu yanayo tuzunguka,"Mkuu wa Mkoa.
"Niwaombe sana viongozi wa dini zoezi hili la chanjo muende mkatusaidie kuwaelimisha wananchi kujitokeza kwa wingi kuwapa chanjo watoto,lengo tufanikishe mpango huu,na kuhusu kipindu pindu mvua bado zipo maeneo yenye mlipuko hasa masoko na mialo miundombinu irekebishwe na usafi uzingatiwe",RAS Balandya.
Mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa amewakumbisha watumishi wa Serikali kutoka sekta mbalimbali kuongeza juhudi ya kushirikiana na siyo kuiachia Idara ya afya pekee kupambana na ugonjwa huo.
Katika kampeni hiyo ya uzinduzi wa chanjo itakayoanza imeambatana na utowaji wa elimu kuhusiana na ugonjwa wa Surua,Rubella na macho mekundu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.