RC MAKALLA AZINDUA MIUNDOMBINU YA ELIMU MRADI WA BOOST ILEMELA
*Amshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha nyingi kwenye miradi ya Elimu*
*Atuma salamu kwa wanafunzi wanaoendelea na mitihani ya kuhitimu Elimu ya Msingi*
*Abainisha kuwa Ijumaa ya Septemba 15, 2023 atazindua mradi mkubwa wa Maji wa Butimba*
*Awataka Ilemela kujivunia uwanja wa Ndege ambao unaboreshwa kuwa wa Kimataifa*
*Akemea utoro kwa wanafunzi na awataka wazazi kusimamia na kuacha kuwaozesha*
*Aagiza sekta ya Ardhi kuweka vigingi (Bicon) kwenye maeneo ya shule ili kuepusha migogoro ya ardhi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.CPA Amos Makalla ameupongeza uongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kutekeleza kwa ufanisi na kwa wakati miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu ya shule za awali na msingi inayotekelezwa na BOOST kwa zaidi ya Bilioni 1.56.
Makalla ametoa pongezi hizo leo Septemba 13, 2023 katika hafla ya makabidhiano ya miundombinu ya shule za awali na msingi zilizotekelezwa kupitia mradi wa BOOST iliyofanyika kwenye shule mpya ya Buteja ambapo amesema uboreshaji huo utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
"Mkoa wa Mwanza kupitia mradi wa BOOST tumepokea zaidi ya Bilioni 12 kwenye Kuboresha miundombinu ya elimu ya msingi, kwakweli huyu Rais ana upendo yaani kila kukicha anamwaga fedha kwenye miradi kedekede kwa Watanzania." Mkuu wa Mkoa.
"Leo nimefarijika maana katika Mkoa wa Mwanza Ilelema mmekua wa kwanza kukabidhi miradi ya Elimu ya BOOST na nitumie wasaa huu kuwashukuru viongozi wote wa wilaya hii wa chama na Serikali kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kusimamia ujenzi wa miundombinu hii kwakweli mmefanya kazi nzuri sana." Makalla.
Halikadhalika, ametumia wasaa huo kukemea tabia ya utoro wa wanafunzi na amewaagiza wazazi kusimama kidete kuhakikisha watoto wanapata elimu bila kukatisha na pia akakemea tabia ya kuozesha watoto kwa tamaa ya kupata fedha kupitia mahari kwani wanakatisha ndoto za watoto.
"Ndugu wazazi nawaomba muitikie wito wa kuhakikisha watoto wetu wanapata chakula wawapo shuleni kwani kinasaidia kuongeza ufaulu na nimewaagiza kuwepo kwa bodi hai za shule ili kuleta ufanisi wa huduma lakini ninyi wazazi na walezi tambueni kuwa mna wajibu wa kushirikiana na juhudi hizo."
Vilevile, ametumia wasaa huo kubainisha kuwa siku ya Ijumaa ya tarehe 15 kesho kutwa historia ingine inaenda kuandikwa kwani atawasha mashine ya mtambo wa kutawanya maji kila kona ya Mkoa huo hivyo wananchi wa Wilaya hiyo wajiandae kwa neema.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemema Mhe. Hassan Masalla amebainisha kuwa ukamilishaji wa miradi hiyo utasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani kwa uwiano unaofaa kuketi kwenye viti meza na kwamba wamekubaliana kuanza kutumia rasmi niundombinu hiyo mara tu shule zitapofunguliwa wiki ijayo.
"Tulikua na uhaba wa madawati zaidi ya Elfu tano ambapo tulifanya jitihada za kutatua kupitia wadau na kwa mradi huu utasaidia kupunguza hadi kubakiwa na uhaba wa madarasa kama elfu mbili tu kwakweli tunamshukuru Mhe. Rais kwa utekelezaji wa miradi mikubwa kwa miaka mitatu mfululizo." Mkuu wa Wilaya.
Adv. Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela amesema vyumba 54 vya madarasa, vyoo matundu 70, majengo 2 ya utawala, Ofisi ya Mwalimu, madawati 1075, Viti 90 na meza 90 vya elimu ya awali, viti 74 na meza 74 za walimu pamoja na miundombinu ya viwanja vya michezo vimegharimu zaidi ya Tshs. 1.56 za mradi wa BOOST.
Kibamba amesema ujenzi wa miundombinu hiyo yote utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na ametumia wasaa huo kumshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuendelea kuboresha huduma za jamii ambazo zimekua zikisaidia kuinua hali ya maisha ya wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa usimamizi wa pamoja wa kina baina ya viongozi wa Wilaya hiyo umesaidia kukamilisha kwa wakati kwa ujenzi ulioanza Mei Mosi mwaka huu na kukamilia Agosti 30 na ametoa shukrani kwa wananchi waliochangia nguvu kazi za zaidi ya milioni 500 kwenye ujenzi huo.
Mhe. Yusuf Bujiku Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilemela amesema kazi hiyo na zingine ni mapenzi ya Mhe. Rais Samia na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020-25 na ametumia wasaa huo kuwaomba wananchi kumuombea afya njema na kumuunga mkono.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.