*RC Makalla azindua msimu mpya wa Pamba, awataka Maafisa Ugani kuwa na shamba darasa*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla leo Novemba 17,2023 amezindua msimu mpya wa Pamba 2023-24 wilayani Magu na kuwataka Maafisa Ugani wote Mkoani humo kuwa na shamba darasa kwa lengo la kuongeza tija wakati wa mavuno.
Akizungumza kwa niaba yake Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Emil Kasagara kwenye kijiji cha Mwalina kata ya Mwamabanza ulikofanyika uzinduzi huo, amesema Serikali imeweka mazingira rafiki kuanzia kwa Maafisa Ugani kwa kuwapatia nyenzo ya usafiri wa Pikipiki hivyo ni wajibu wao kuhakikisha malengo ya kupata mavuno zaidi yanafikiwa.
"Malengo ya Mkoa wetu msimu huu huu wa 2023-24 ni kulima hekta 60,178 kupata mavuno ya tani 45,457,mpango huu utakuja na matokeo chanya endapo wakulima watapata elimu ya kutosha kutoka kwenu wataalamu",Kasagara.
Amewataka wakulima wa Pamba kuzingatia ushauri wa kitaalamu huku Serikali ikiwa tayari imewawekea mazingira mazuri kuanzia bei nafuu ya mbolea na mbegu bora na kuwasisitiza kuondokana na ukulima wa kimazoea ambao matokeo yake ni kuvuna Pamba hafifu na zisizo na ubora.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi wa bodi ya Pamba James Shimbe amebainisha msimu huu wamehakikisha kila kitu kimefika kwa wakati kwa mkulima ili afanye maandalizi mazuri ya Kilimo cha Pamba.
"Hadi kufika tarehe 15,Novemba 2023 jumla ya tani za mbegu ya Pamba 1,682 zimepelekwa kwenye Halmashauri zinazolima Pamba kati ya hizo Tani 1,394 zimegawiwa kwa wakulima",Shimbe
"Tumekuwa na mafanikio katika kilimo cha Pamba kwa misimu 3 mfululizo ikiwemo Pembejeo kuletwa kwa wakati,uzalishaji kuongezeka mwaka hadi mwaka kuanzia 2019 hadi 2023, na kuimarika kwa huduma za Ugani,"Emmanuel Siyo,mratibu wa zao la Pamba Mkoa wa Mwanza.
Mkoani Mwanza zao la Pamba linalimwa zaidi kwenye Halmashauri za Misungwi,Magu,Kwimba,Sengerema na Buchosa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.