RC MAKALLA : USIKILIZZAJI KERO ZA ARDHI BILA UTATUZI NI KAZI BURE
*Asema Maafisa Ardhi wanafeli kwenye Mambo Matano*
*Awataka Maamuzi ya utatuzi migogoro ardhi yafanyiwe kazi*
*Awataka maafisa ardhi kusimamia sheria za ardhi ili kutenda haki kwa wananchi*
*Aagiza maafisa ardhi kutoa maamuzi ya maandishi kwa rejea ya baadae*
*Awataka maafisa hao kutowazungusha wananchi wanapohitaji huduma*
*Aagiza ulipaji wa fidia ili kuondoa migogoro kwenye maeneo yaliyotwaliwa*
*Atangaza ziara ya 2 kusikiliza Jimbo kwa Jimbo, awali amesikiliza kero 926*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amewataka watumishi wa sekta ya ardhi mkoani humo kufuata sheria na miiko ya kazi yao ili kutenda haki kwa wananchi pamoja na kuepusha migogoro ya ardhi ikiwa ni pamoja na kumaliza migogoro iliyobainika kwa kufikia maamuzi.
Ametoa agizo hilo leo 07 Machi 7, 2024 wakati akifungua kikao kazi cha watumishi wa sekta ya ardhi kinachowakutanisha wataalamu hao kutoka kwenye Halmashauri za mkoa huo katika ukumbi wa halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
"Nawaomba twendeni tukafanye kazi kwa mujibu wa sheria, ipo mifano ya kutolewa hati kwenye ardhi juu ya hati ingine yaani hata ukisikia unajiuliza huyu afisa aliyetoa hati hii ni wa aina gani jamani, nendeni mkafanye kazi kwa kufuata taratibu kwa weledi mkubwa," amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Katika kutatua kero za wananchi, Makalla amewataka kutoa maamuzi kwa maandishi ili kupata rejea ya kudumu kwenye hatua zilizopitia hadi kutatua kero ikiwemo utoaji fidia kwa maeneo yaliyotwaliwa kwa ajili ya kumbukumbu kwa miaka ya baadae na akawataka kuacha urasimu kwenye utoaji huduma.
Kamishna Msaidizi wa ardhi Mkoa wa Mwanza Bi. Happyness Mtutwa amebainisha kuwa kikao kazi hicho ni mahususi kwa ajili ya kukumbushana misingi ya utoaji huduma kwa wananchi kupitia sekta ya ardhi na kwamba watumishi 126 walioajiriwa na 146 wa mkataba wamekutana.
"Mhe. Mkuu wa Mkoa huu ni muendelezo wa utatuzi wa kero za ardhi kwa watumishi wa ardhi na tumeitana kwa ajili ya kukumbushana miiko, taratibu na misingi ya utendaji kazi kwenye sekta yetu na kuepuka rushwa na kuwa na weledi wakati wote." Amesema Kamishna Msaidizi.
Bi. Mtutwa amefafanua kuwa kupitia zoezi la usikilizaji wa kero za wananchi lililofanywa na Mhe. Mkuu wa Mkoa mwishoni mwa mwaka jana na kuagiza utatuzi wa haraka tayari wamemaliza migogoro 86 na kwamba hati 4206 zimetolewa ndani ya muda huo mfupi kwa wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa wananchi 570 wamesikilizwa kupitia kliniki ya Jijini Mwanza, 132 Usagara-Misungwi na 262 Ilemela na kwamba kupitia maduhuli wamekusanya Bilioni 5.6 ndani ya muda huo wa takribani miezi sita ya uendeshaju wa kliniki za kusukiliza kero.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.