RC MAKALLA ZIARANI SENGEREMA APONGEZA UJENZI WA MIRADI, AHIMIZA WAZAZI KUPELEKA WATOTO SHULE
*Awapongeza Halmashauri kusimamia ujenzi wa madarasa kwa muda mfupi*
*Awataka wananchi kuchukua tahadhari ya Kipindupindu, aagiza kutolewa elimu*
*Awataka viongozi kushirikiana kuhamasisha wazazi kupeleka watoto shule*
*Awataka wananchi kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya maendeleo*
*Awapongeza TANROADS kuunganisha wananchi kupitia daraja la Bugakala*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwa kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya madarasa kwa ubora na ufanisi mkubwa hususani shule mpya za Sekondari kwenye kata za Misheni na Nyampulukano.
Mhe. Makalla ametoa pongezi hizo leo Januari 15, 2024 wakati alipokua wilayani humo kwa ukaguzi wa miradi ya maendeleo, uandikishaji wa wanafunzi na ufuatiliaji wa maagizo yake aliyoyatoa wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi, kufuatilia uandishikishaji wa wanafunzi na kukagua miradi ya maendeleo.
Makalla amesema pamoja na ujenzi huo amebaini kuwepo kwa shule zilizosajili wanafunzi wengi hadi kwa asilimia 106 lakini uwepo wa shule zenye idadi ndogo ya wanafunzi waliosajiliwa kujiunga kidato cha kwanza, darasa la kwanza na awali na kufuatia hali hiyo ameagiza walimu kufanya uhakiki na kushirikiana na wazazi kuhakikisha watoto wanawasili shule.
Akiendelea na ziara hiyo kwenye miradi mbali mbali Mhe. Mkuu wa mkoa amewataka TARURA na TANESCO kufanya tathmini ya gharama za kupeleka huduma hizo kwenye shule mpya na kuwasilisha kwenye uongozi wa halmashauri ya Sengerema ili iweze kulipia na kuhakikisha maabara, madarasa na miundombinu mingine inapata huduma safi.
Vilevile, ametumia wasaa huo kuwataka viongozi na watendaji wilayani humo kushirikiana katika kutoa elimu kwa jamii ya maradhi ya ugonjwa wa kipindupindu na kuhakikisha kila anapopatikana mgonjwa mwenye dalili hizo basi apelekwe hospitali mapema iwezekanavyo akapate huduma hiyo ya bure huku akibainisha kuwa kuna wagonjwa 74 na mmoja akifariki.
Akikagua ujenzi wa jengo la Mamlaka ya mapato linalojengwa kwa zaidi ya Bilioni 2.3 wilayani humo, Mhe. Mkuu wa Mkoa amewataka taasisi hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kulipa kodi kwa hiyari na kuwataka wao kama watendaji kutenda haki katika kukisia na kutoza kodi huku akibainisha kuwa mkoa huo unaoshika nafasi ya pili Kitaifa kuchangia pato la Taifa umekusudia kukusanya zaidi.
Halikadhalika, amewapongeza TANROADS kwa kuwaunganisha wananchi wa Sengerema na Nyangh'hwale mkoani Geita kupitia daraja la Bugakala lililojengwa kwa Milioni 650 ambapo amesema lilisababisha hadi vifo kutokana na kina kirefu cha maji na kwamba daraja hilo jipya litasaidia kusafirisha mazao na biashara.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.